Saturday, January 29, 2022

Mkoa wa Singida wadhamiria makubwa kwenye utunzaji wa Mazingira.

 Wananchi Mkoani Singida wameaswa kutumia mbinu mbadala za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na athari za mabadiliko ya Tabianchi ili kupata  Mazingira  Safi na kuondoa uwezekano wa kupata Upungufu wa chakula katika ngazi ya Kaya.

Mbinu hizo zimetajwa kuwa ni upandaji wa miti ili  kutunza Mazingira na kuleta mvua pamoja na kilimo cha uwele na mtama aina ya Serena hasa katika kipindi hiki ambacho Mamlaka ya Hali ya hewa imebainisha kwamba  mvua zitanyesha chini ya wastani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa upandaji miti ngazi ya mkoa uliofanyika katika pembezoni mwa ziwa Kindai na.Munangi , Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Pasksi Muragili ambaye amemuwakilisha RC Singida katika kazi hiyo amesema ili kupambana na changamoto ya mabadiliko ya Hali ya hewa lazima kila Kaya ipande miti kuanzia miwili katika maeneo yao na kwa wakulima walime mtama aina ya Serena ili kujipatia chakula cha kutosha.

Amesema ilikuwa utaratibu wa Mkoa kufanya usafi kila Siku ya Jumamosi lakini kwa sasa usafi huo utafanyika kila Siku huku Jumamosi ikitumika kama Siku ya kupanda miti mpaka mvua itakapofikia kikomo.

DC Muragili amefanya kwamba ni jukumu la kila mtu, Halmashauri na Manispaa mbalimbali hapa Singida kuhakikisha miti inapandwa inalelewa na inalindwa dhidi ya mifugo na baadhi ya watu wasiokuwa na nia njema ya utunzaji wa mazingira.

Akizungumza kuhusu usafi Mgeni rasmi huyo amesema kuanzia sasa Manispaa ianze kuwashughulikia wote ambao watatupa takataka hovyo badala ya kutumia vizimba vilivyotengwa maeneo mbalimbali ya mjini.

Aidha, DC Muragili akaagiza kila mkulima ahakikishe analima ekari moja anayoipanda mtama  aina ya Serena kwa kuwa unastahimili ukame na unatoa mazao mengi, mazao mengine ni kama uwele huku alisisitiza watu kufanya kazi kwa bidii.

Naye Kaimu Mkuu wa Idara ya Mazingira Bi Shuku Kaishwa  akitoa taarifa yake kwa mgeni rasmi amesema  ni Mpango wa Manispaa kuhakikisha kila Taasisi inapewa eneo la kudumu la kupanda miti na kuitunza ili kuifanya Singida kuwa ya kijamii.

Aidha Shuku amebainisha kwamba kupitia Manispaa wameandaa Mpango wa kuhamasisha jamii  na taasis kuanzisha mashamba ya Miche pamoja kueleza jamii faida zitokanazo na mazao ya miti pamoja na   upandaji wa miti aina ya mihimbo katika vyanzo vya maji.

Afisa Mazingira huyo amatoa wito kwa  jamii ya wafugaji na wataalamu wa mifugo kuendelea kuielimisha jamii juu ya ufugaji wa ndani (zero Grazing) ili kuepuka kusambaza kwa mifugo nje na kujaribu miti iliyopandwa huku akiwataka wananchi kuhamasika na kuanza kutumia nishati mbadala ambao utapunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na  wakuu wa Idara mbalimbali ngazi ya Mkoa na Halmashauri,kamati ya ulinzi na usalama, taasisi mbalimbali watumishi wa umma, wanafunzi na wananchi mbalimbali.

Mkuu wa Wilaya ya Singida akishiriki zoezi la upandaji miti lililofanyika Ki Mkoa leo 29/1/2022 katika fukwe za Ziwa Kindai na Munangi Singida Mjini

Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kiaratu akipanda mti wakati wa zoezi hilo la lililofanyika Kimkoa leo

Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida Zefrin Lubuva akishiriki zoezi la upandaji miti 

Mfanyakazi wa Shirika la Tree for the Future lenye makao yake makuu mkoani Singida akishiriki zoezi la upandaji miti lililofanyika kimkoa

Wawakilishi wa Shirika la TTCL kwa pamoja wakishiriki zoezi la upandaji miti 



No comments:

Post a Comment