Wednesday, November 10, 2021

Miradi ya Ujenzi wa vyumba vya madarasa, Hospitali na visima vya maji kukamilishwa kabla ya Desemba 10, 2021 - RC SINGIDA

Bodi za shule za msingi na sekondari pamoja na Madiwani katika kata mbalimbali mkoani Singida wametakiwa kuwashirikisha wananchi katika Ujenzi wa vyumba vya madarasa, Hospitali na visima vya maji ili kukamilisha Ujenzi huo kabla ya Desemba 10, 2021.

Mkuu wa Mkoa Singida Dkt. Binilith Mahenge  ametoa kauli hiyo leo tarehe 8.11.2021 alipotembelea Ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Sekondari ya Manyoni iliyopo wilayani humo na kukuta wafanyakazi na  mafundi wachache jambo ambalo halikumfurahisha.

"Katika Wilaya nyingine wananchi wamehamasika ambapo walichimba msingi na kusaidia kusogeza mchanga  kokoto na zege  na kusaidia kufanya kazi kwenda kwa haraka, sasa hapa kuna mafundi watatu hawawezi kumaliza kazi hii kwa wakati.” Alisema Dkt.Mahenge

Dkt Mahenge amesema Mpango uliopo ni kuhakikisha vyumba 662 vya madarasa kwa sekondari na Msingi shikizi kwa mkoa kukamilika kabla ya Decemba 15 mwaka huu na endapo kazi hiyo itashindikana kukamilishwa kwa namna yoyote ile wasimamizi wanaohusika waajiandae kufukuzwa kazi.

Hata hivyo amezitaka Bodi za shule kuhakikisha kwamba wanawashirikisha wananchi katika Ujenzi huo na kuacha kudhani kwamba hela hizo zitatosha kwa kila kitu.

Aidha amesema wadau wanaruhusiwa kuchangia  baadhi ya vitendea kazi ikiwemo mchanga, kokoto au nguvu kazi kwa kuwa  kila darasa lilikadiriwa kutumia kiasi cha sh.Milion 20 kwa kila darasa.

Amemtaka Mkurungezi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kuhakikisha wananunua vifaa kwa pamoja ili kupunguza gharama ikiwa ni pamoja na kutoa Oda mapema kwa kuwa mahitaji ni makubwa ambapo kila mkoa vinahitajika.

"Nataka mjiongeze hakutakuwa na msamaha kwa yeyote atakayesababisha wanafunzi kukosa madarasa wakati hela tayari zimeshatolewa, sitahitaji kusikia eti vifaa viliisha, ndio maana nasema mjiongeze mtoe oda mapema."Alikaririwa Mkuu wa Mkoa.

Naye Alhaji Juma Kilimba Mwenyekiti wa CCM Mkoa akawataka viongozi wote wa chama Mkoa, Kata na tarafa kuhakikisha wanasimamia na kuhimiza wananchi kushiriki nguvu kazi ili kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wanapata madarasa ifikapo tarehe 15 Desemba mwaka huu.

Pia amewataka mafundi wote mkoani hapo waliochaguliwa kufanya kazi hizo kuongeza idadi ya mafundi na vibarua ili kazi zisikwame na ziweze kukamilika kwa wakati.


Mkuu wa Wilaya hiyo Rahabu Magesa, akasisitiza kwamba wamejipanga kutembea mashule yote ambayo wanaendelea na Ujenzi wa vyumba vya  madarasa ili kusimamia na kuhakikisha zoezi linafanikiwa kama ilivyopangwa.


No comments:

Post a Comment