MATUMAINI
ya kurejea kwa kilimo cha umwagiliaji katika skimu ya Itagata iliyopo wilayani
Itigi mkoani Singida yameanza kujitokeza kwa Wakulima baada ya kuanza
kutekelezwa kwa maagizo ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge
ya kuvunja uongozi uliokuwepo na kuchukuliwa kwa mashamba ambayo
hayaendelezwi katika skimu hiyo.
Ikiwa ni mwezi mmoja umepita baada ya mkuu wa mkoa
kutembelea skimu hiyo na kuwataka wakulima kuchagua uongozi mpya ambao
utashirikiana na viongozi mbalimbali kufanya tathmini ya ugawaji na uendelezaji
wa mashamba, Oktoba 23, 2021 kwa mara nyingine ametembelea skimu hiyo na kukuta
wamechagua viongozi wapya na tathmini ya mashamba imefanyika.
Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara na wakulima hao Mahenge
amemshukuru mkuu wa wilaya hiyo, Rahabu Magesa na viongozi wengine kwa
kuanza kutekeleza maagizo yake na kuwaeleza kwamba hatua hiyo iwe
endelevu na kuhakikisha wakulima wanafuata sheria na taratibu za skimu hiyo.
“Skimu hiyo iligharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.2 tokea
ilipoanza kujengwa mpaka mwaka 2019 ilipokabidhiwa kwa kijiji husika, ni lazima
lazima usimamizi ufanyike ili uzalishaji uongeze iweze kutoa mchango kwa taifa”
alikaririwa Dkt. Mahenge.
Aidha Dkt. Mahenge akiwa kijijini hapa akatoa wito kwa wakulima
wote wenye umiliki wa mashamba katika skimu hiyo kulipa ada zinazotakiwa
ambazo zitatumika kukarabati miuondombinu ya skimu pale itakapo hitajika.
Hata hivyo Rc huyo alisema ulinzi wa miundombinu ya skimu
ni jukumu la kila mwananchi hivyo akawakumbusha watu wenye makazi ndani ya
Skimu kuhakikisha wanafuata sheria zilizowekwa kwenye skimu hiyo kama
wakishindwa watalazimika kuhama.
Aidha maagizo hayo yametokana na malalamiko yaliyowasilishwa na
Afisa Kilimo kwamba wakazi hao wamekuwa wakiwatishia wakulima wengine wakidai
eneo hilo lipo chini yao jambo ambalo limeleta kero kwa wakulima wengine.
Akijibu maswali ya wananchi ambao wametakiwa kulipia ada wakati
mashamba yao hayajafikiwa na miundombinu ya umwagiliaji na kufanya kilimo chao
kutengemea mvua za msimu Mahenge akaendelea kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa
Halmashauri hiyo kuhakikisha miundombinu inatengenezwa maeneo yenye changamoto
ya kufikisha maji ili wakulima waweze kumwagilia .
“Nataka tuelewane kwamba kila mkulima ndani ya skimu anahaki
sawa na mkulima mwingine hivyo kila mtu anatakiwa kufikiwa na maji na kutoa ada
kulingana na ukubwa wa anachokimiliki”.aliendelea kufafanua Mahenge.
DC wa wilaya hiyo Rahabu Mwagisa alisema kwa sasa wakulima hao
wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji ila Serikali inaendelea
kuwaunganisha na wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za kifedha ili kupata
mikopo
Rahabu akawashauri wakulima hao kulima mpunga kwa kuwa
soko lake ni la uhakika na watakao amua kulima matunda au mbogamboga
wahakikishe wanalima kwa wingi kwa ajili ya kulitosheleza soko.
Awali Afisa kilimo wa kijiji cha Itagata Bi. Halima
Issingo alibainisha kwamba skimu hiyo ina ukubwa wa ekari 400 zinazofaa kwa
kilimo na inauwezo wa kulisha wilaya nzima endapo itafanya kazi kwa viwango
vyake vyote.
Afisa kilimo huyo alisema jumla ya ekari 209 kati ya 400
zimegawiwa kwa wanachama na kati hizo ekari 115 ndizo zililzolimwa
mpunga na kutoa tani 120.75 wakati ekari 26 zililimwa mahindi na kutoa
tani 14.4
Alisema moja ya mipango ndani ya skimu ni kufikisha miundombinu
ya umwagiliaji katika maeneo ambayo hayana ili kuifanya skimu nzima iweze
kuzalisha vya kutosha.
Wakulima nao wakapata nafasi ya kutoa maoni baada ya mkutano
ambapo Musa Saidi mkulima wa skimu hiyo wameishukuru Serikali kwa hatua
walioichukua ya kuhuisha skimu hiyo na kuomba wataalamu waendelee kutoa elimu
kwa wakulima ili kubadilisha mazingira ya uzalishaji na kulima ki biashara.
Michaeli Simuli Ngawe mkulima wa mpunga naye akiomba Serikali kuwaletea mbolea na mbegu za kisasa za mpunga kwa kuwa wengi wao hawatumii mbolea na mbegu bora kwa kuwa dhamiara ya serikali na wakulima kwa sasa ni kubadilisha kilimo kiwe chenye tija.
Mkuu wa mkoa akisikiliza kero mbalimbali kutoka kwa wakulima wanaotumia skimu ya Itagata mara baada ya kumaliza mkutano wa hadhara.
No comments:
Post a Comment