MKUU wa mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi,
ameziagiza ofisi zote za halmashauri za wilaya mkoani Singida kuanzia sasa,
ofisi za watendaji Kata zitakuwa vituo vya kupokea taarifa za changamoto
mbalimbali zinazohusu sekta ya kilimo.
Dkt. Nchimbi, ametoa agizo hilo hivi karibuni wakati
akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya mkopo wa mbegu bora za alizeti aina
ya Hysun 33, tani sita kwa wakulima wadogo Tarafa ya Mtinko halmashauri ya
wilaya ya Singida, zilizotolewa na
shirika la Faida MaLi la jijini Arusha lenye tawi lake mkoani Singida.
Amesema lengo la kuanzisha vituo hivyo, ni
kuharakisha kuzitafutia ufumbuzi wa changamoto hizo kabla hazijaanza kuleta
madhara makubwa.
Akifafanua zaidi, mkuu wa mkoa huyo ameeleza, pindi ofisi hizo zitakapokuwa zikipokea taarifa za changamoto mbalimbali zinazokabili
sekta ya kilimo kwenye maeneo mbalimbali, ni budi kuziwahisha kwenye mamlaka
husika ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu mapema.
“Serikali ya awamu ya tano imeweka lengo la Tanzania kuwa
ya viwanda na uchumi wa kati. Hatuwezi kufikia lengo hilo endapo hatutaweka
mkazo mkubwa kwenye sekta ya kilimo”,
“Kuanzia sasa, nawataka Maafisa kilimo na ugavi, wahamishie
ofisi zao mashambani kwa wakulima, wasisubiri wakulima wawafuate, wenyewe ndio
wawafuate wakulima huko mashambani”. Amesema Dkt. Nchimbi.
Aidha, Dkt. Nchimbi amesisitiza kuwa, hataki
kusikia afisa kilimo au afisa ugani ameshindwa kwenda shambani kwa wakulima kutokana
na mvua kunyesha.
“Utawasikia wataalam hawa wa kilimo wakiombea mvua
inyeshe kidogo kisha ikatike. Hakuna cha mvua kukatika…, mvua itawakatikia hukohuko
mashambani. Mvua ni neema na ni baraka kutoka kwa Mungu. Naomba mvua isikimbiwe
na wala isisingiziwe”, Dkt. Nchimbi.
Amesisitiza kuwa, Mheshimiwa Rais Dkt. John
Magufuli amehimiza viongozi na watendaji wajiamini katika kutatua kero za
wananchi, na wananchi hao wafuatwe huko huko waliko.
Aidha, Mkuu wa mkoa huyo ameahidi Serikali yake ya mkoa
wa Singida itaendelea kushirikiana na shirika la Faida MaLi, MIVARF, ByTrade
(T) Ltd, SDC na TADE katika kusaidia upatikanaji wa mbegu bora.
Hata hivyo, amemuagiza Afisa Kilimo wa mkoa
kushirikiana na wasaidizi wake kuandaa kalenda ya kilimo cha mazao mbalimbali
na kuzisambaza kwenye taasisi zikiwemo za madhehebu ya dini, akieleza kuwa,
kazi ya kilimo ina Baraka kutoka kwa Mungu.
“Kilimo ni kazi ambayo Mungu ameibariki, na kila
mwaka kilimo kinakuwa na nafasi nyingi za ajira. Mungu amekuwa akitoa Baraka zake
kwenye kilimo kwa kukipa mvua za kutosha kama ambazo zinanyesha msimu huu”.
“Kwa hiyo, viongozi wa dini wakipata kalenda ya
kilimo cha mazao mbalimbali, watatenga muda wa kuwakumbusha waumini wao umuhimu
wa kazi ya kilimo. Nina uhakika wakulima waumini watazingatia muda stahiki wa
kila zao kwa ajili ya kupanda mbegu bora. Kwa njia hii kilimo kitakuwa na tija
zaidi na kitaharakisha kufikia uchumi wa kati” Dkt. Nchimbi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shirika la Faida MaLi, Bw. Tom
Silayo, amesema mbegu ya alizeti ya aina ya Hysun 33, ilijaribiwa mwaka jana na
kutoa magunia 18 ya alizeti ghafi kwa ekari moja (1) ikilinganishwa na gunia
nne (4) kama ilivyozoeleka.
“Msimu huu tumehamasisha wakulima wapatao 20,460 kutumia mbegu
hii ya Hysun 33. Tunachukua na tumeorodhesha majina na namba zao za simu. Wajibu
wetu mwingine ni kuhakikisha tunakuza masoko endelevu. Lengo likiwa ni wakulima
waendelee kupata faida zaidi ili mwisho wa siku waishi maisha yaliyo bora”.
Amesema Silayo.
Naye, Mkulima mdogo Bi. Amina Dafi, pamoja na kulishukuru
shirika la Faida MaLi amesema, kuanzia msimu huu wataondokana na matumizi ya
mbegu za mazoea (mbegu hasara), na kutumia mbegu bora walizokopeshwa ili waweze
kupata mavuno mengi yatakayosaidia kuinua uchumi wao.
Zao la alizeti ni malighafi katika viwanda 144 vya kukamulia
mafuta mkoani hapa. Viwanda hivyo vinahitaji tani 482,500 za alizeti ili viweze
kufanya kazi kwa kipindi cha mwaka mzima.
Kauli
mbiu ya mwaka huu ya kilimo cha alizeti inasema,
“ALIZETI SINGIDA - BADILI GIA,
TUMIA MBEGU BORA”.
“kauli mbiu hii naomba iwe ni wimbo wa kila siku kwa wakulima
mkoani Singida”. Dkt. Nchimbi.
MATUKIO KATIKA PICHA
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi kushoto akisalimiana na Katibu Tawala wa wilaya ya Singida DC Bw. Wilson Shimo mara baada ya kuwasili kwenye hafla ya makabidhiano ya mkopo wa mbegu bora za alizeti aina ya Hysun 33, tani sita kwa wakulima wadogo Tarafa ya Mtinko halmashauri ya wilaya ya Singida.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi kushoto akisalimiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Singida DC, Bw. Rashidi Mandoa mara baada ya kuwasili kwenye hafla ya makabidhiano ya mkopo wa mbegu bora za alizeti aina ya Hysun 33, tani sita kwa wakulima wadogo Tarafa ya Mtinko halmashauri ya wilaya ya Singida.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi kushoto akisalimiana na Mkurugenzi wa shirika la Faida MaLi, Bw. Tom Silayo, mara baada ya kuwasili kwenye hafla ya makabidhiano ya mkopo wa mbegu bora za alizeti aina ya Hysun 33, tani sita kwa wakulima wadogo Tarafa ya Mtinko halmashauri ya wilaya ya Singida.
Mbegu bora za alizeti aina ya Hysun 33, tani sita zilizokopeshwa kwa wakulima wadogo Tarafa ya Mtinko halmashauri ya wilaya ya Singida.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Singida DC, Bw. Rashidi Mandoa akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya mkopo wa mbegu bora za alizeti aina ya Hysun 33, tani sita kwa wakulima wadogo Tarafa ya Mtinko halmashauri ya wilaya ya Singida.
Mkurugenzi wa shirika la Faida MaLi, Bw. Tom Silayo akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya mkopo wa mbegu bora za alizeti aina ya Hysun 33, tani sita kwa wakulima wadogo Tarafa ya Mtinko halmashauri ya wilaya ya Singida.
Bw. David Vallence kutoka Kampuni ya ByTrade ambao ni wasambazaji wa mbegu Hysun 33 (Chotara), akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya mkopo wa mbegu bora za alizeti aina ya Hysun 33, tani sita kwa wakulima wadogo Tarafa ya Mtinko halmashauri ya wilaya ya Singida.
Mkuu wa wilaya ya Singida DC, Mhandisi Paskasi Muragili akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya mkopo wa mbegu bora za alizeti aina ya Hysun 33, tani sita kwa wakulima wadogo Tarafa ya Mtinko halmashauri ya wilaya ya Singida..
IMETOLEWA NA;
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO
OFISI YA MKUU WA MKOA
SINGIDA
No comments:
Post a Comment