Tuesday, January 15, 2019

WATENDAJI MKOANI SINGIDA WATAKIWA KUANZISHA VITUO VYA MKONO KWA MKONO KUOKOA WAANGA WA UKATILI


Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi akifungua kikao kazi cha kuandaa jumbe za kuelimisha jamii kuhusu ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya watoto kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bw. Sebastian Kitiku na wa kwanza kushoto ni Bw. Christopher Mushi Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii.

.............
KATIBU Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi amewataka watendaji wa Serikali mkoani Singida kuanzisha vituo vya Mkono kwa Mkono (One Stop Centres) ili waanga vitendo vya ukatili waweze kupata huduma kwa haraka tofauti na sasa wanapokumbana na mlolongo wa taratibu unaochangia kupotea kwa ushaidi.

Dkt. Lutambi ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa kikao chake na baadhi ya watendaji wa mkoa wake wanaotengeneza JUMBE za kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii.

Aidha Dkt. Lutambi amewataka watendaji hao kutengeneza jumbe ambazo zitatoa elimu pamoja na mambo mengine yatakayowezesha waanga wa ukatili kupata mahali pakukimbilia, jambo lililomladhimu  kuwaagiza kuanzisha vituo vya mkono kwa mkono kwa lengo la kuwapatia huduma ya haraka waanga hao.

Aidha, ametaja urasimu  na taratibu ngumu zinazojitokeza baada ya muanga wa ukatili kufika katika vituo vya polisi ambapo waanga wanalazimika kufuata PF3 kituo cha polisi pamoja na kufuata milolongo ya kumuona daktari jambo ambalo linasababisha baadhi ya waanga kukata tamaa na wengine kurubuniwa na kubadili mawazo. 

Dkt. Lutambi pia amewataka ndugu, pamoja na raia wema kushirikiana na madawati ya Jeshi la Polisi kutokomeza kabisa vitendo vya ukatili kwa kutoa ushaidi mahakamani kwani kesi nyingi mahakamani zinakwama kutokana na kukosa ushahidi.

Kwa mantiki hiyo, amewataka watendaji hao kuweka mifumo imara itakayowezesha watendaji na waanga wa ukatili kufanikisha kukomesha vitendo vya ukatili sio tu kwa Mkoa wa Singida bali pia Tanzania kwa ujumla.

Wakati huo huo Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Watoto kutoka Wizara ya Afya, Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bw. Sebastian Kitiku wakati akiongea na vyombo vya habari, ameitaja mila ya ukeketaji kama mojawapo ya mila inayopaswa kuachwa kwa kuwa inaacha makovu ya kisaikoloijia kwa mtu anayepata kufanyiwa tohara lakini pia ina madhara katika suala zima la Afya ya uzazi, kwani mlengwa anaweza kupoteza maisha wakati wa kujifungua.

Mkurugenzi huyo amewataka wananchi mkoani Singida kubadilika kifikra na kuacha vitendo vya ukatili ambavyo kwa mazingira ya ulimwengu wa kisasa hayana nafasi tena.

 Mkurugenzi Msaidizi Idara ya watoto kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bw. Sebastian Kitiku akiongea wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha watendaji wa Mkoa pamoja na Wizara ya Afya kujadili jumbe za kuelimisha jumii kuhusu ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Kushoto kwake ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi na wa kwanza kulia ni Bw. Patrick Kasango Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu, mkoa wa Singida.

 Kikao kikiendelea


Bw. Christopher Mushi, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii akiwasilisha mada "UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO TANZANIA".

 Picha ya pamoja

IMETOLEWA NA;
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO
OFISI YA MKUU WA MKOA
SINGIDA


x

No comments:

Post a Comment