Friday, November 30, 2018

KILELE CHA MAADHIMISHO YA WIKI YA MSAADA WA KISHERIA TAREHE 30 NOVEMBA, 2018 SINGIDA

HOTUBA YA MHESHIMIWA SELEMANI JAFFO(MB),WAZIRI OFISI YA RAIS –TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA WIKI YA MSAADA WA KISHERIA TAREHE 30 NOVEMBA, 2018 SINGIDA
Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb), Waziri wa Katiba na Sheria,
Mh.Dkt.Rehema Nchimbi, Mkuu wa Mkoa wa Singida,
Prof. Sifuni Mchome, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria,
Ndugu. Amon A. Mpanju, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria,
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya Mliopo,
Waheshimiwa Wabunge mliopo,
Waheshimiwa Madiwani mliopo,
Wadau wa Maendeleo,
Wawakilishi wa Mashirika Wahisani,
Viongozi na Wakuu wa Mashirika na Taasisi zinazotoa Msaada wa Kisheria,
Mawakili wa Serikali mliopo hapa,
Mawakili  wa Kujitegemea,
Waheshimiwa Mahakimu mliopo,
Watumishi wa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali mliopo,
Watoa huduma ya Msaada wa Kisheria
Wasaidizi wa Kisheria,
Waandishi habari
Mabibi na Mabwana

Habari za Asubuhi.

Ndugu waalikwa, Naomba mniruhusu kwa namna ya kipekee sana kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai, kutujalia afya njema na hata kutuwezesha kukutanika hapa siku ya leo.
Ndugu waalikwa, Kwa namna ya pekee napenda kumshukuru Mheshimiwa Prof. Palamagamba J.A.M Kabudi(Mb), Waziri wa Katiba na Sheria na uongozi wa Wizara kwa kunialika nije kuwa mgeni wa heshima katika kilele cha wiki hii ya msaada wa kisheria nchini.
Ndugu waalikwa,  maadhimisho haya yalifunguliwa rasmi Tarehe 26, Novemba,2018 Mjini Morogoro na Mhe. Waziri wa Katiba na Sheria na kwa wiki nzima huduma za msaada wa kisheria zimekuwa zikitolewa kwa wananchi.
Ndugu Waalikwa, ni jambo la kihistoria kwa Serikali kujikita katika suala hili na nichukue fursa hii kuipongeza Serikali kwa hatua hii muhimu katika kuwasaidia wananchi wasio na uwezo kupata huduma wanayostahili ya msaada wa kisheria ambayo ni haki yao na hivyo kuweza kuifikia haki.
Ndugu waalikwa, Sisi sote ni mashahidi wa nia ya dhati ya Serikali katika kuhakikisha wananchi wasio na uwezo wanawezeshwa kupata huduma ya msaada wa kisheria. Haya yote yanafanyika ili kumuwezesha mwananchi kuifikia haki kama anavyostahili aweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za Maendeleo na hivyo kuwezesha ndoto ya serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wakati na viwanda ifikapo mwaka 2025.
Kama mnavyofahamu maadhimisho ya mwaka huu yanaenda na kauli isemayo Huduma ya Msaada wa kisheria iwakumbuke akina mama na watoto”  hii ina maana kuwa tunatambua kuwa jamii yenye kudumu katika migogoro ni jamii inayojijengea umaskini kwani hukosa muda wa kufanya shughuli za kujiingiza kipato; na hivyo harakati za kuinua uchumi wa nchi  na kufikia azma ya kukukua kiuchumi hatuwezi kuzifikia kwani wananchi wengi hasa wanawake na watoto katika jamii husika wanakosa haki zao kwa kushindwa kupata msaada wa kisheria na hivyo kuendelea kuwa wanyonge mbele ya jamii inayowazunguka.

Kwa mantiki hii, kauli mbiu hii inaikumbusha jamii na wadau wengine wa haki nchini kuhakikisha wanawake na watoto wanapata msaada wa kisheria ili kuwasaidia kupata haki pale wanapostahili kwani wengi wao wanakosa haki hata kama wanastahili kwa kukosa msaada wa kisheria na hawana uwezo wa kuwa na mawakili ili kuwasaidia kupata haki pale wanapostahili.
Jambo la muhimu katika tukio hili la leo ni kuwasisitizia washiriki na watoa huduma za msaada wa kisheria nchini kuhakikisha wanatoa kipaumbele kwa kuwapatia wanawake na watoto Msaada wa Kisheria kwa kuimarisha mapambano na vitu au vikwazo vinavyowafanya wanawake na watoto kupata huduma za msaada wa kisheria nchini ili kuweza kupata haki kwa wakati.

Ndugu waalikwa, Kama mnavyofahamu Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na wizara yangu imedhamiria kufikisha huduma za msaada wa kisheria karibu kabisa na wananchi ambapo iliteua wasajili wasaidizi kwa nchi nzima na kuwapatia mafunzo juu ya Sheria ya Msaada wa Sheria Na. 1 ya mwaka 2017 ili waisimamie na kuitekeleza kwa kuwasajili watoa huduma za msaada wa kisheria katika wilaya na halmashauri zote nchini ili huduma hiyo itolewe na kupatikana kwa ufanisi.
Ndugu Waalikwa, Hayo yote yanafanyika kwa njia ya kuimarisha utawala wa sheria na kuhakikisha kuwa hata wale wasio na uwezo wanapata huduma hii.Msaada wa Kisheria unabeba dhana nzito ya kupeleka huduma kwa wananchi bure na bila malipo yoyote. Kwa kupeleka huduma hii kwa wananchi wa kawaida,  utawala wa sheria unaimarishwa na unaongeza upatikanaji wa haki sawa kwa wote na kwa wakati hasa kwa wananchi masikini. Na nichukue nafasi hii kuwapongeza wote mnaopeleka msaada wa kisheria kwa wananchi na kuhakikisha huduma hii inapatikana kikamilifu.
Ndugu waalikwa, Napenda kuwafahamisha wadau wote kuwa Serikali ya Awamu ya Tano  inatambua kuwa wako wananchi wenye uhitaji wa msaada wa kisheria katika mashauri ya jinai na madai. Sheria ya Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017 inatoa pia majukumu kwa Mahakama ya kuamuru mtuhumiwa au mdaawa ambaye Mahakama itaona anastahili kupata msaada wa kisheria apatiwe huduma hiyo.
Ndugu waalikwa, Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha inatekeleza matakwa ya Sheria hii kwa kuandaa Kanuni za Maadili na Miongozo ya Watoa Huduma, kuandaa mitaala ya mafunzo ya wasaidizi wa kisheria nchini ambao kwa mujibu wa Sheria hii wanatambulika rasmi. Nimefahamishwa kuwa hivi sasa wataalamu wanaaendelea na mafunzo ya msaada wa kisheria kwa askari polisi na askari magereza kwa nchi nzima ili waweze kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi mbalimbali watakao hitaji huduma hiyo katika maeneo wanayofanyia kazi nchini. Hizi zote ni jitihada zinazochukuliwa na Serikali na wadau wake katika utekelezaji wa Sheria ya Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017.
Ndugu Waalikwa, Ninashukuru sana uongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria kwa ushirikiano na Mahakama na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kuona umuhimu wa kuweka utaratibu huu mzuri wa ushirikiano na ninawaahidi kuwa Wizara yangu itafanya kila liwekanalo kusukuma mbele jitihada za Serikali kuwafikia wananchi wenye uhitaji wa msaada wa kisheria.
Ndugu Waalikwa, Kasi na ari iliyooneshwa na watoa huduma ya msaada wa Kisheria katika maadhimisho haya ni kielelezo kuwa Sheria hii mpya ya Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017 ni mkombozi kwa jamii ya wasio na uwezo wa kumudu gharama za mawakili. Kitendo cha kuwatambua Wasaidizi wa Kisheria katika Sheria hii kimewapa moyo na ari ya kutoa huduma kwa wananchi. Ni jukumu letu sasa kuwatambua na kuwatumia katika maeneo yetu. Ninafahamu kuwa Wasaidizi wa Kisheria ni watu waliopo karibu sana na jamii kuliko vyombo vingi vya dola. Ninafahamu pia kwamba wenzetu kutoka nchi jirani kama Malawi walianza kuwatumia Wasaidizi wa Kisheria miaka mingi iliyopita na sasa migogoro mingi inatatuliwa pasipo kufika Mahakamani. Huu ni utamaduni mzuri ambao tunapaswa kuuiga. Masuala mengi yanayofika Mahakamani yangeweza kabisa kumalizika kwa usuluhishi katika ngazi ya familia, ukoo au mtaa kama tu pangekuwa na fursa ya wadaawa kukutanishwa kama walivyokuwa wanafanya wazee wetu hapo zamani na jamii ikaendelea kuishi kwa amani na utulivu.

Ndugu waalikwa, ni matarajio yangu kuwa tufike mahali kama Watanzania tuheshimu maamuzi ya mahakama kuhusu haki zetu na haki za wengine; tujali zaidi utu kuliko tabia ambazo zinatusababishia migogoro kama ya urithi; tuheshimu mipaka ya ardhi zetu ili tusijiingize kwenye migoro ya ardhi; na kuheshimu mikataba na makubaliano tunayoingia ili tusiingie katika madai ya kuvunja Mikataba. Wasaidizi wa Kisheria watatusaidia sana kwenye kuelimisha jamii haki zao na kuturejesha katika utamaduni uliotufikisha kuwa Kisiwa cha amani katika Ukanda uliogubikwa na migogoro.

Mheshimiwa Waziri na Waalikwa;Naomba nitumie fursa hii kuzungumzia suala la maadili ya watoa huduma za msaada wa Kisheria na ubora wa huduma. Itakuwa si jambo zuri kuwa na mfumo mzuri wa kisheria ikiwa huduma yenyewe inayotolewa itakuwa sio bora na watoa huduma watakuwa hawakidhi vigezo. Wasaidizi wa Kisheria watapoteza sifa ya kutegemewa, kuheshimiwa na kuthaminiwa endapo wachache wao watakosa nidhamu na maadili na kushindwa kuheshimu dhamana waliyopewa. Watoa huduma waepuke kutumia nafasi zao ili kujinufaisha au kuwa mawakala wa ukiukwaji wa maadili na vitendo vya rushwa au udanganyifu.

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana; Leo tunahitimisha wiki hii muhimu sana kwa wananchi kujipatia huduma hii ambayo imetolewa kwa wiki nzima katika mkoa huu na mikoa mitano mingine nchini na katika maeneo ya vizuizi ikiwa pamoja na polisi na magereza. Ni rai yangu kwa wananchi wote kuendelea kutumia fursa zilizopo za kupata ushauri wa kisheria na sio kusubiri mpaka mwakani kipindi kama hiki.
Wageni waalikwa, Kwa mara nyingine tena, napenda kutoa shukrani za dhati kwa washirika wetu wa maendeleo ambao wamekuwa nasi bega kwa bega katika kuhakikisha shughuli hii. Naomba niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu ili Sheria hii itekelezwe ipasavyo.
Baada ya kusema hayo, niwakumbushe kuwa Huduma ya Msaada wa Kisheria iwakumbuke akina mama na watoto”

Ndugu Waalikwa, Nichukue fursa hii kuwaambia kuwa maadhimisho haya ya Wiki ya Msaada wa Kisheria Nchini kwa mwaka 2018 nimeyamefunga rasmi.
 ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA.

No comments:

Post a Comment