Thursday, May 05, 2016

MKUU WA MKOA AMSIMAMISHA KAZI MKURUGENZI KWA KUMDANGANYA KUHUSU WATUMISHI HEWA.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Singida Simon Mumbee aliyesimamishwa kazi na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew Mtigumwe amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Singida Simon Mumbee kwa kumdanganya kuhusu watumishi hewa katika halmashauri yake.

Mtigumwe ametoa maagizo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dokta Angelina Mageni Lutambi ya kumwandikia barua ya kumsimamisha kazi Mkurugenzi huyo leo asubuhi kwakuwa alitoa taarifa kuwa serikali haikupata hasara yoyote kutokana na watumishi hewa 20 waliopatikana katika halmashauri yake.

Ameongeza kuwa baada ya uchunguzi kufanyika imebainika kuwa serikali ilipata hasara ya shilingi milioni 125 kutokana na watumishi hewa waliopatikana katika halmashauri ya Singida.

Mtigumwe amesema Watumishi hewa  Mkoani Singida ni 231 ambao wameisababishia serikali hasara ya shilingi milioni 146.2 na pia ameagiza zoezi la kuwatambua watumishi hewa lifanyike tena kuanzia tarehe 9 Mei, 2016.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Singida amempa onyo Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida Joseph Mchina kutokana na kauli zake kwa wateja wake.

Mtigumwe amemuelekeza mkurugenzi huyo kujirekebisha na kuwasikiliza wananchi, aidha amewaelekeza wakurugenzi wote kuwatumia watendaji husika kutatua kero za wananchi akitoa mfano wa kuwatumia maafisa ardhi katika kupanga maeneo na kutatua migogoro ya ardhi.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe.

No comments:

Post a Comment