Wednesday, April 27, 2016

WAZIRI WA MAJI AAHIDI KUWATUMBUA VIONGOZI WATAKAOHUJUMU MIRADI YA MAJI

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Injinia Gerson Lwenge akipampu maji katika moja kati ya visima 12 vilivyochimba  na Tigo katika kijiji cha Mtinko, Singida.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Injinia Gerson Lwenge amesema hatawaonea huruma bali atawachukulia hatua za kisheria watendaji na viongozi watakaohujumu miradi ya maji.

Waziri Lwenge ameyasema hayo leo wakati akipokea visima 12 kutoka kwa kampuni ya simu za Mkononi ya Tigo katika kijiji cha Mtinko Wilayani Singida.

Amesema watendaji na viongozi wanapaswa kusimamia miradi ya maji ili ahadi ya Raisi wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe John Pombe Magufuli ya kufikia asilimia 80 ya wananchi wa vijijini kwa huduma za maji safi na salama ifikapo 2020, itimie.

Waziri Lwenge ameiagiza halmashauri ya Singida kusimamia uundwaji wa kamati ya  jumuiya za watumia maji katika kila  kijiji chenye visima hivyo na kuzisimamia ili mapato yatumike kuendeleza miradi ya maji.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew Mtigumwe amemuahidi Waziri Lwenge kusimamia watendaji wake ili miradi ya maji iweze kuwanufaisha wananchi wa Singida, na kuwasihi wananchi wa Singida kufuata maelekezo ya Waziri Lwenge ya kutunza miundombinu na kuchangia miradi ya maji.

Mhandisi Mtigumwe amemuomba Waziri kuweka kipaumbele kwa Mkoa wa Singida katika bajeti ya wizara ili ipate miradi mingine ya maji kwakuwa mkoa wa Singida unapata mvua kidogo kiasi cha milimita 500 mpaka 800 kwa mwaka.

Mkurugenzi wa Tigo kanda ya Kati George Lugata amesema kampuni yake imechimba visima 12 katika wilaya za Singida, Iramba, Manyoni na Ikungi Mkoani Singida vikiwa na thamani ya shilingi milioni174.

Baadhi ya wakazi wa Mtinko wameishukuru kampuni ya Tigo na serikali kwa kuwaletea huduma ya maji kwakuwa itapunguza kero ya maji na hivyo kuwapa muda wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo.
 
 Amina Saidi na Halima Ally wamesema hapo awali wamekuwa wakitumia muda mwingi kutafuta maji na hivyo kuathiri shughuli za uzalishaji mali na kulea familia hivyo kisima hicho kutawapunguzia kero hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew Mtigumwe akipampu maji katika moja kati ya visima 12 vilivyochimba  na Tigo katika kijiji cha Mtinko, Singida.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Injinia Gerson Lwenge akimsaidia kubeba ndoo ya maji Amina Saidi Mkazi wa Mtinko.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Injinia Gerson Lwenge akipanda mti katika moja kati ya visima 12 vilivyochimba  na Tigo katika kijiji cha Mtinko, Singida.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Injinia Gerson Lwenge akipanda mti katika moja kati ya visima 12 vilivyochimba  na Tigo katika kijiji cha Mtinko, Singida.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Injinia Gerson Lwenge akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mtinko, Singida.

No comments:

Post a Comment