Monday, April 25, 2016

VIKAO VYA KISHERIA VISISUBIRI POSHO-MKUU WA MKOA WA SINGIDA

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Injinia Mathew Mtigumwe amefanya ziara katika Wilaya za Mkalama na Iramba ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo Machi 18 mwaka huu.

Mbali na kutumia  ziara hiyo kujitambulisha kwa watendaji mbalimbali wa wilaya hizo,  Mtigumwe alitumia fursa hiyo kusisitiza watendaji hao kufanya kazi kwa bidii ili kuendana na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa John Pombe Magufuli ambapo aliwataka kuhakikisha wanafanya kazi mara mbili au tatu ya walivyokuwa wakifanya kipindi hicho.

“Kama tunalipwa mishahara kutoka kwenye kodi za wananchi, hatuna budi kuhakikisha tunamaliza kero zote ambazo zinawakabili ili waweze kufanya kazi kwa nguvu na kuongeza kipato” Alisema Mtigumwe.

Alisema watendaji wote wa serikali ni lazima watimize wajibu wao kikamilifu na kama kuna kikao cha kisheria kwa ajili ya kujadili shughuli za maendeleo ni lazima kikae  bila kungoja posho.

“Nimeagiza ndani ya miezi miwili  idara zote za  mashauri ya walimu (TSD), zikae vikao na kusikiliza mashauri yote yanayowahusu  walimu” Aliongeza Mtigumwe.

Akisisitiza juu ya hilo Mtigumwe alisema kama kuna mtu wa TSD ambaye hayupo tayari kukaa kwenye vikao hivyo mpaka apate posho aandike jina lake kwa mkuu wa Wilaya ili atafutwe mtu ambaye yupo tayari kusikiliza na kutatua kero za walimu.


“Hata madiwani pia, kama mnatakiwa kukaa vikao vya kisheria msisubiri posho, kaeni alafu pesa ikikusanywa mtalipwa. Nchi haiwezi kwenda kwa kusubiri posho muda wote na naomba posho zote ambazo si za kisheria ila tulikuwa tukilipana baada ya mapato ya halmashauri kuwa makubwa zisitishwe rasmi” Aliongeza.
 
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Injinia Mathew Mtigumwe akisalimiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mkalama  Ndugu Bravo K. Lyapembe mara baada ya kuwasili Wilayani hapo nyuma yake (aliyevaa kaunda suti) ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mheshimiwa Christopher Ngubiagai.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Injinia Mathew Mtigumwe akisaini vitabu vya wageni katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mara baada ya kuwasiliWilayani hapo.
Watendaji na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba wakimsikiliza kwa umakini Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Injinia Mathew Mtigumwe (hayupo pichani).
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Injinia Mathew Mtigumwe akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Watendaji wa Wilaya ya Mkalama. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. James Nkwega. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Christopher Ngubiagai akifuatiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Ndugu Bravo K. Lyapembe na wa mwisho ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkalama Ndugu Benjamin Mwombeki. Waliosimama ni waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.

No comments:

Post a Comment