Sunday, March 08, 2015

UKEKETAJI KWA WATOTO WACHANGA WAFANYIKA KIJIJI CHA SEPUKA WILAYANI SINGIDA.
Baadhi ya akina mama wa kijiji cha Sepuka wakifuatilia semina ya kupinga ukeketaji kwa mtoto wa kike iliyoandaliwa na shirika la Women Wake Up (WOWAP).

Wakazi wa Kijiji cha Sepuka wilayani Singida wameiomba Serikali kwa kushirikiana na mashirika binafsi yaendelee kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya ukeketaji kwa watoto wa kike kwani jamii hiyo bado inaendelea kukeketa watoto wa kike wakiwa wachanga.

Wakazi hao wametoa rai hiyo wakichangia mada katika semina iliyoandaliwa na shirika la Women Wake Up (WOWAP) linaloendesha mradi wa Kutokomeza ukeketaji kwa njia ya majadiliano ya vikundi kwa ufadhili wa shirika la Japan la Women Action Against FGM(WAAF JAPAN).
 
Nasra Suleimani Afisa ufuatiliaji na tathmini na Samora Mnyawonga kutoka WOWAP wakizungumza na wakazi wa Sepuka juu ya madhara ya ukeketaji kwa mtoto wa kike.

Wamesema ukeketaji bado unafanyika kwa siri sana kwa kushirikiana na ndugu wa karibu mfano bibi au shangazi huku wanaume wakiwa wamefichwa juu ya suala hilo.

Wameongeza kuwa ndugu wenye umri mkubwa kama bibi na shangazi huwashawishi akina mama kukeketa watoto wachanga kwa kisingizio kuwa kutampunguzia mtoto uwezekano wa kupata magonjwa ya mara kwa mara.

Baadhi ya wanaume walioshiriki semina hiyo wamesema kuwa wamepata elimu ya madhara ya ukeketaji na wako tayari kuwalinda watoto wao na wengine dhidi ya ukeketaji.

Wameongeza kuwa ukeketaji bado unaendekezwa na wazee kwakuwa jamii ya sasa imeshaelimika hivyo nguvu zaidi ielekezwe kwa wazee ambao huwashawishi akina mama, aidha wameiomba serikali kuweka utaratibu wa kutoa elimu ya madhara ya ukeketaji katika kliniki za ujauzito.

Samora Mnyawonga kutoka WOWAP wakizungumza na wakazi wa Sepuka juu ya madhara ya ukeketaji kwa mtoto wa kike.

Kwa upande wake mwezeshaji ambaye ni mratibu wa mradi huo Zuhura Karya amewataka akina mama na wanaume waliopata elimu hiyo wawe mabalozi wa kupinga ukeketaji kwa mtoto wa kike na ukatili wowote, pia watoe taarifa katika vyombo vya usalama wapatapo taarifa za ukeketaji.

Karya amewashauri akina mama kuangalia usafi wa mtoto mchanga kwa kuhakikisha nepi za watoto zinakuwa safi, usafi wao na wa chakula cha mtoto  ili kuwakinga watoto wachanga dhidi ya magonjwa na sio kuwakeketa.
Mwezeshaji ambaye ni mratibu wa mradi wa kutokomeza ukeketaji kwa njia ya majadiliano ya vikundi Zuhura Karya (mwenye miwani) akiwaelimisha wakazi wa Sepuka juu ya madhara ya ukeketaji.

No comments:

Post a Comment