Friday, February 13, 2015

WATENDAJI WAAGIZWA KUFUTA AIBU YA KUFANYA VIBAYA KATIKA UCHANGIAJI WA CHF NA TIKA MKOANI SINGIDA.


Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan akifungua kikao cha uhamasishaji wa uchangiaji wa CHF na TIKA Mkoani Singida kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko V. Kone.

Watendaji katika Halmashauri tatu za Manispaa, Singida na Mkalama Mkoani Singida wameagizwa kufuta aibu ya kufanya vibaya katika uchangiaji wa mifuko ya afya ya jamii ya CHF na TIKA kwa kuwa wana fursa na uwezo wa kufanya vizuri.

Agizo hilo limetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko V. Kone wakati akifungua kikao cha uhamasishaji wa uchangiaji wa Mifuko ya afya ya jamii ya CHF na TIKA Mkoani hapa.

Hassan amesema Halmashauri tatu zimekuwa zikifanya vizuri katika uchangiaji wa CHF na kuufanya Mkoa wa Singida kuongoza kitaifa katika uchangiaji wa mifuko hiyo ya afya ya jamii huku Halmashauri nyingine tatu zikifanya vibaya.

Amesema taarifa ya utekelezaji wa CHF inayoishia Disemba 31, 2014  inaonyesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba ina wanachama hai 33,502, Manyoni wanachama 20,859, Ikungi wanachama 13,042, Singida wanachama 10,167, Mkalama wanachama 7,662 na Manispaa ya Singida wanachama 6,918.


Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan akiwa na Mwenyekiti wa Kikao cha uhamasishaji wa CHF na TIKA Mkuu wa Wilaya ya Singida Mwl. Queen M. Mlozi, wa mwisho ni Kaimu Meneja wa Bima ya Afya Mkoa wa Singida Bw. Adam Salum.

Naye Mwenyekiti wa Kikao cha uhamasishaji wa CHF na TIKA Mkuu wa Wilaya ya Singida Mwl. Queen M. Mlozi amewaasa waganga wakuu wa wilaya kuacha utendaji wa ofisini bali watembelee vituo vilivyoko chini yao ili kupata takwimu sahihi na kusimamia maadili ya watoa huduma za afya. 

Mlozi amesema huduma bora ikiwa ni pamoja na uhakika wa dawa katika vituo ya huduma za afya na hospitali vitawavutia wananchi wengi kujiunga na CHF na TIKA bila ya kutumia nguvu nyingi za ushawishi.Kaimu Meneja wa Bima ya Afya Mkoa wa Singida Bw. Adam Salum akifafanua jambo kuhusu mifuko ya afya ya jamii ya CHF na TIKA kwa wajumbe.Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida Zuhura Karya akichangia katika kikao cha uhamasishaji wa uchangiaji wa mifuko ya afya ya jamii ya CHF na TIKA.

Akichangia katika kikao hicho Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida Zuhura Karya amezitaka halmashauri za Mkoa wa Singida kuweka mikakati bora ya kusaidia makundi maalumu katika jamii kama vile walemavu, wazee na watoto kujiunga na CHF na TIKA.


Nao baadhi ya wajumbe wa kikao hicho wamewashauri wanasiasa kusaidia makundi maalumu kama vile wanafunzi kuwalipia CHF na TIKA kuliko kugawa vitu vingine kwa jamii.

Aidha Halmashauri zote zimeshauriwa kuhakikisha zinatenga bajeti kwa ajili ya uhamasishaji wa kujiunga na CHF na TIKA, kuboresha huduma za afya ili wanachama waongezeke na waliojiunga wasitamani kujitoa na kuhakikisha matumizi ya pesa za CHF na TIKA zinatumiwa kwa mujibu wa taratibu.

Baadhi ya wajumbe waliohudhuria kikao cha uhamasishaji wa uchangiaji wa mifuko ya afya ya jamii ya CHF na TIKA.

No comments:

Post a Comment