Wednesday, January 07, 2015

MREMBO WA KANDA YA KATI ATOA MSAADA WA MASHINE ZA KUPUMULIA KWA HOSPITALI YA MKOA WA SINGIDA.



Redds Miss Kanda ya Kati 2014/15, Doris Mollel akiwaona watoto njiti baada ya kukabidhi mashine mbili za kupumulia watoto waliozaliwa kabla ya muda wa kawaida kwa Hospitali ya Mkoa wa Singida.

Katika kuianza safari yake ya huduma za jamii kwa mwaka 2015, Redds Miss Kanda ya kati 2014-2015 Doris Mollel ametoa msaada wa mashine 2 za kupumulia kwenye hospitali ya Mkoa wa Singida zenye thamani ya Tsh 1,200,000/=.
Mashine hizo huwasaidia watoto waliozaliwa kabla ya muda wa kawaida (Pre-mature babies) katika mfumo wao wa upumuaji ambao huhitaji msaada wa juu zaidi mara tu wanapozaliwa.
Doris ambaye pia ni mshindi wa tatu wa Redds Miss Tanzania 2014 ni mwanaharakati wa dhana ya Urembo wenye Malengo endelevu kwa jamii ‘Beauty with a Purpose’.
Redds Miss Kanda ya Kati 2014/15, Doris Mollel akizungumza mara baada ya kukabidhi mashine mbili za kupumulia watoto waliozaliwa kabla ya muda wa kawaida kwa Hospitali ya Mkoa wa Singida.
Aidha amefanya kazi kubwa kwenye sekta ya elimu akijikita zaidi kwenye kuchangia Vitabu kwa shule za msingi na sasa, akiwa ni mmoja ya watu ambao walizaliwa kabla ya muda wa kawaida ameamua kupanua wigo wake wa huduma za jamii kuleta mwamko na kusaidia kuokoa maisha ya watoto hawa.

Akiongea kwenye hafla ya kukabidhi mashine hizo iliyofanyika hospitalini hapo, Mollel alisema. “Kiwango cha vifo kwa watoto wanaozaliwa kabla ya kukomaa ni karibu 30% vikichangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa vifaa vya kutosha kusaidia mifumo yao ya upumuaji mara tu wanapozaliwa. Nikiwa moja ya watoto hao ambaye nilibahatika kupata msaada na huduma ya kutosha nilipozaliwa, Ninaelewa ni jinsi gani matunzo haya ya awali yalivyo muhimu kwenye kuokoa maisha ya watoto hawa na ninajikita kuwasaidia”.

Naye Bw. Albert Mbepera, Mkurungezi wa Manifester brand amesema ‘huduma kwa jamii ni eneo muhimu sana kwetu, tunafurahi kujitolea kufanya kazi na Doris katika maswala ya kusaidia jamii na tunaamini kuwa ushirikiano huu utasaidia kukusanya na kuonyesha matatizo ya wahitaji ili kuongeza uelewa na msukumo wa misaada kutoka kwa sekta binafsi na wanajamii kwa ujumla’

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mkuu wa wilaya ya Singida Mwl. Queen Mlozi na ilihudhuriwa na Mganga mfawidhi wa hospitali ya Mkoa wa Singida Bw. Daniel Tarimo, Daktari bingwa wa watoto wa Hospitali ya Singida, Muandaaji wa Redds Miss Singida 2014 Bora Lemmy na washindi wengine wa Redds Miss central Zone.

Mgeni rasmi kwenye hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Singida Mwl. Queen Mlozi akiwa katika picha ya pamoja na Redds Miss Kanda ya Kati 2014/15, Doris Mollel pamoja na waalikwa wengine.


Picha na Habari kwa Hisani ya Moblog !!!!

No comments:

Post a Comment