Friday, December 05, 2014

KIKAO CHA KAMATI YA USHAURI YA MKOA (RCC)


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko Vicent Kone akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Social Training Centre mjini Singida

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dokta Parseko Vicent Kone, amewahimiza wananchi waliojiandikisha kwenye daftari la wapiga kura, wajitokeze na kushiriki kwenye mikutano ya kampeni ili kujijengea mazingira mazuri ya kuchagua viongozi bora.

Dokta Kone ametoa wito huo jana wakati akifungua kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Social training centre mjini Singida.
 
Amesema mikutano hiyo ya kampeni ni mahali wagombea wa ngazi mbalimbali za uongozi wanapotangaza sera zao hivyo basi hapo ndipo mahali pekee wananchi wanaweza kujua uwezo wa uongozi wa mgombea na iwapo sera zake zinagusa vipaumbele vyao.

“Nawasisitiza wananchi wajitokeze na kushiriki kwenye mikutano ya kampeni kwa amani na utulivu na watoe taarifa mapema kwenye vyombo vya usalama wanapohisi au kuona baadhi ya wananchi wakitaka kuvuruga amani au kutaka kutekeleza vitendo vya uvunjifu wa amani”, amesema Dokta Kone.

Dokta Kone ameongeza kuwa matarajio ya wananchi ni kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika kama ulivyopangwa na hatimaye kuwapata viongozi ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa kwa amani na utulivu.

Katika hatua nyingine, Dokta Kone ametumia fursa hiyo kuwakumbusha viongozi na watendaji kuhakikisha wanafunzi waliofaulu, wanajiunga na kidato cha kwanza mwakani bila kukosa.
“Isitokee mwanafunzi kubaki nyumbani kwa kushindwa kuhudhuria shule aliyopangiwa”, alisisitiza.

Aidha Dokta Kone ametoa takwimu za kilimo kwa msimu wa mwaka 2013/2014 ambapo kwa mazao ya chakula jumla ya tani 913,143 zimezalishwa ikilinganishwa na lengo la kuzalisha tani 780,420, wakati uzalishaji wa mazao ya biashara umefikia tani 363,005.


Baadhi ya wajumbe wa kikao cha ushauri mkoa wa Singida wakifuatilia ajenda za kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Social Training Centre mjini Singida.(Taarifa na Nathaniel Limu).

No comments:

Post a Comment