Monday, November 24, 2014

MAADHIMISHO YA SIKU YA MLIPA KODI YAFANA MKOANI SINGIDA.

Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone, akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya mlipa kodi Mkoa wa Singida yaliyofanyika kwenye ukumbi wa askofu Mabulla mjini Singida. Wa kwanza kulia ni Kaimu meneja wa TRA Mkoa wa Singida, Samwel Shula na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Queen Mlozi.
 
Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Singida, imekusanya zaidi ya shilingi 4.14 bilioni kuanzia julai mwaka jana hadi sasa, ikiwa ni ongezeko la asilimia 34  ikilinganishwa na shilingi bilioni 3.09 zilizokusanywa kwa kipindi hicho katika mwaka wa fedha uliopita.

Aidha,wigo wa kodi umeongezeka kwa kuandikisha walipa kodi kutoka 5,821 mkwa 2012/2013 hadi kufikia walipakodi 6,859 kwa mwaka 2013/2014. 

Hayo yamesemwa na kaimu meneja TRA mkoa wa Singida, Samwel Shula wakati akitoa taarifa yake kwenye kilele cha maadhimisho ya nane ya siku ya mlipa kodi yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa askofu Mabula mjini Singida.

Kaimu meneja wa TRA Mkoa wa Singida, Samwel Shula, akitoa taarifa kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya mlipa kodi Mkoa wa Singida. Maadhimisho hayo yamefanyika kwenye stand ya askofu Mabula mjini Singida. Wa pili kulia (waliokaa) Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dokta Parseko Kone, anayefuata ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Queen Mlozi na Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Liana Hassan.

Akifafanua zaidi,alisema katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 hadi kufikia mwezi wa oktoba mwaka huu,lengo lilikuwa kukusanya shilingi 1.55 bilioni na mkoa umeweza kukusanya shilingi 1.59 bilioni ikiwa ni kiwango cha utendaji cha aslimia 102.

“Napenda kutambua mchango mkubwa wa walipa kodi wote na wadau mbalimbali katika eneo hili la kulipa kodi na kwenda sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu;”Risiti ni haki yako,asiyetoa anakwepa kodi”, alisema.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dokta Parseko Kone, alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la ukusanyaji wa mapato kuliko ili ya ukuaji wa uchumi katika kipindi chote ambacho TRA imekuwa msimamizi wa jukumu hili la kukusanya mapato ya serikali kuu.

“Nawapongeza viongozi na watumishi wote wa TRA na wadau wote kwa mafanikio haya.Ninatambua kuwa mafaniko haya ni matokeo ya juhudi na nguvu za watu wengi,wote nawapongeza sana”,alisema Dokta Kone.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dokta Parseko Kone, (katikati) akimkabidhi cheti cha mdau wa TRA Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Liana Hassan. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Singida. Queen Mlozi na kulia ni Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Singida, Samwel Shula.

Katika hatua nyingine, Dokta Kone amewakumbusha wafanyabiashara kujenga utamaduni wa kutoa risiti pindi wanapouza bidhaa mbalimbali na pia wanunuzi nao waone fahari kudai risiti kwa bidhaa walizonunua.

Aidha ameiasa TRA mkoani hapa kuongeza juhudi za kukusanya mapato zaidi na wakati huo huo wahimize utaratibu wa kulipa kodi kwa hiari na kuanzisha mifumo rahisi na rafiki kwa mlipa kodi. Hii ni pamoja na matumizi sahihi ya mashine za kieletroniki za kutolea risiti (EFD).


Baadhi ya wafanyabiashara na wadau wa TRA Mkoa wa Singida, waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya siku ya mlipa kodi yaliyofanyika kwenye stand ya askofu Mabula mjini Singida.






(Picha/taarifa na Nathaniel Limu-dewjiblog).

No comments:

Post a Comment