Tuesday, September 05, 2023

SERIKALI YATUMIA ZAIDI YA SH. BILIONI 17.8 KUBORESHA MIUNDOMBINU ELIMU YA AWALI NA SHULE ZA MSINGI, SINGIDA

Mkoa wa Singida umepokea zaidi ya Sh. Bilioni 17.8, kutoka Serikali Kuu kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na 2022/2023, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya elimu ya awali na shule za msingi ili kumwezesha mwanafunzi kupata elimu bora zaidi darasani.   

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mosses Machali akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba wakati wa uzinduzi wa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto (PJT-MMMAM).

Hayo yamebainishwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mosses Machali wakati wa uzinduzi rasmi wa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto (PJT-MMMAM-2021/22-2025/26), huku Serikali ikiyapongeza mashirika 19 kati ya 59 yaliyosajiliwa kwa kutekeleza moja kwa moja programu hiyo mkoani Singida.

Mashirika mengine 40 kati ya 59 ambayo makao makuu yake yapo mkoani Singida na mengine nje ya mkoa yanatekeleza kazi zake kupitia miradi mbalimbali ikiwemo afya, elimu, maji, ujenzi wa miundombinu, ulinzi na usalama, lishe na usafi wa mazingira.

Serukamba amefafanua kuwa, kati ya fedha hizo, Shilingi 6,925,704,502/24 zililetwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu msingi kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na kiasi kingine cha Shilingi 10,925,465,901/34, kimetumika kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga akizungumza wakati wa uzinduzi wa Programu huyo.

Mkuu huyo wa mkoa alifafanua kuwa, ili kuhakikisha mtoto anakuwa kwenye utimilifu wake, Serikali ya awamu ya sita imewekeza katika kuboresha uhai wa mtoto kupitia utoaji wa huduma bure za afya kwa mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

Amefafanua kuwa, Serikali imewekeza katika elimu ya awali kwa kuwajengea uwezo walimu wa ufundishaji kutengeneza na kutumia zana malezi na makuzi kwa walimu 151 wa elimu ya awali, walimu wakuu 21 na maafisa elimu kata 21 kwa mwaka 2022/2023.

Awali akizindua Programu hiyo kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, amesema kuwa, Programu hiyo ni kielelezo tosha cha Rais Samia Suluhu Hassan, katika kujali malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga akizungumza wakati wa uzinduzi wa Programu huyo.

“Mpango huu wa MMMAM umelenga kuwekeza mapema kwa mtoto kwa kuwa ukuaji unaanza wakati wa kutungwa mimba hadi miaka nane ambacho ni kipindi cha ukuaji zaidi. Programu hii imelenga kwenye maeneo makuu matano ambayo ni afya bora, lishe ya kutosha, malezi yenye mwitikio, ujifunzaji wa awali na ulinzi na usalama,”alifafanua

“Ni dhahiri kabisa, lishe bora katika jamii ni kichocheo cha maendeleo katika nyanja zote, ikiwemo afya, kilimo, elimu, biashara na uchumi…hivyo ni pale tu ambapo athari za lishe duni au utapiamlo zitakapodhibitiwa au kutokomezwa ndipo malengo ya maendeleo katika nyanja hizi yataweza kufikiwa kwa ufanisi,”alisema Serukamba.




No comments:

Post a Comment