Wednesday, April 05, 2023

Chuo cha VETA kijengwe Manyoni - RC Serukamba

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba leo tarehe 5 Aprili, 2023 amemaliza mgogoro wa eneo kitakapojengwa Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kufikia maamuzi kwamba chuo hicho kujengwa katika eneo la Manyoni Makao makuu ya Wilaya.

Maamuzi hayo ameyatoa katika  kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na kuwakutanisha wenyeviti wa Halmashauri zote za Wilaya hiyo, Wabunge wa Manyoni, Madiwani wa Halmashauri ya Itigi na Manyoni, Kamati ya Siasa ya Wilaya na ya Mkoa na Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na mkoa.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akisisitiza jambo wakati wa kikao hicho.

RC Serukamba alipitisha uamuzi wa Chuo hicho kujengewa katika eneo la Setelite Manyoni karibu na eneo la mnada  baada ya kuwahoji Madiwani wa upande wa Manyoni na Itigi na kubaini kwamba hapakuwa na ushirikishwaji katika upatikanaji wa eneo lililopendekezwa mwanzoni ambalo ni Kintiku Lusilile.

Madiwani pamoja na Wabunge walilazimika kupiga kura ya wazi kwamba ili kuamua chuo hicho kujengewa wapi kati ya Kintinku, Lusilile au Manyoni Setalite ambapo kura 10 zilitaka kijengwe Lusilile, 4 zilitaka kijengwe Itigi na kura 32 zilitaka kijengwe Manyoni.

Aidha Serukamba alieleza kwamba eneo hilo lipo katikati hivyo ni rahisi kufikiwa na wananchi wa maeneo yote ya Wilaya hiyo,

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akisoma na kutoa taarifa ya kura zilizopigwa na wajumbe kwaajili ya kuchagua eneo litakapojengwa chuo cha VETA katika Wilaya ya Manyoni wakati wa kikao hicho.

"Maoni ya wengi ni Maoni ya Mungu kwa kuwa wengi wameona chuo hicho kijengwe Manyoni lazima tufanye hivyo ili kiweze kuwasaidia wananchi kutoka pande zote, na wote naomba tuweze kusimamia hili," Alisema Serukamba

Hata hivyo amemuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo kuhakikisha eneo hilo linapimwa na wakabidhiwe Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati kwa ajili ya kuanza hatua za Ujenzi.

Hata hivyo amewataka Viongozi wa Wilaya hiyo kuandaa ziara katika kata zilipotakiwa kujengwa chuo hicho na kuwaelimisha sababu za msingi za kuhamishwa ujenzi huo.

Awali Mkurugenzi wa VETA kanda ya Kati John Mwanja, alieleza sifa ya eneo linalotakiwa kujengwa chuo cha VETA kwamba lisiwe na migogoro, kusiwepo na fidia lisiwe chini ya ekari 20.

MATUKIO KATIKA PICHA

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (kushoto) akimsikiliza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Mhe. Jumanne Shabani Mlagaza, wakati akitoa maoni yake kuhusu eneo litakapojengwa chuo cha VETA wilayani Manyoni.

Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati Dodoma, John Mwanja akitoa ufafanuzi kuhusu sifa za eneo linalopaswa kujengwa chuo cha VETA wakati wa kikao hicho kilichoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida.

Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Kemilembe Lwota, akizungumza wakati wa kikao hicho.

Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, Dkt.Pius Chaya akizungumza wakati wa kikao hicho.

Mbunge wa Manyoni Magharibi Yahaya Masare, akizungumza wakati wa kikao hicho.



Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akisikiliza maoni na kura za Wajumbe ambao ni Waheshimiwa Madiwani wa pande mbili Halmashauri ya  Wilaya ya Manyoni na Itigi wakati wa kikao hicho.


Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na Itigi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida wakati akizungumza katika kikao hicho.

Kikao kikiendelea

No comments:

Post a Comment