Tuesday, February 28, 2023

Chongolo amfagilia RC Serukamba.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amepongezwa kwa jitihada zake za kusikiliza na kutatua kero za Wananchi  wa Mkoa huo jambo ambalo Katibu Mkuu wa CCM Taifa Daniel Chongolo, amesema haijawahi kuona toka amechukua nafasi hiyo.

Akitoa pongezi hizo leo katika mkutano na wananchi wa kijiji cha Solya alipotembelea Mradi wa ujenzi wa shule ya vipaji ya wasichana  na Manyoni mjini alipokuwa akizindua tawi la chama hicho Chongolo amesema kwamba Mkuu wa Mkoa huo amekuwa akikutana na wananchi kila Wilaya kwa kila mwezi ambapo anawasikiliza na kutatua kero zao.

Chongolo alieza kufurahishwa kwake na wananchi wa Solya ambapo alitoa nafasi ya kuuliza maswali na hapakuwa na mwananchi yeyote aliyekuwa na swali wala kero ambapo alielezwa kuwa wananchi huwa wanatoa kero zao kwa Mkuu wa Mkoa kila mwezi mara moja.

Aidha amewaagiza viongozi wote wa Serikali pamoja na Chama kuhakikisha wanaiga mfano huo wa kuwatembelea wananchi kusikiliza kero na kuzitatua badala ya kusubiri ujio wa wageni wakubwa.

"Sijawahi kuona toka nimekalia kiti hiki sehemu ambayo tunakutana na wananchi wakose kuuliza maswali, kwa ukweli nimpongeze Mkuu wa Mkoa huu kwa kazi kubwa anayoifanya ya kusikiliza na kutatua kero za Wananchi ambapo nimeona akifanya mikutano kila mwezi katika Wilaya mbalimbali, naomba tuige mfano huu nchi nzima" alisema Chongolo.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa alitumia muda huo kumuomba Katibu huyo waletewe fedha kiasi cha TSH Bilioni Moja iliyobaki ili iweze kukamilisha Ujenzi wa shule hiyo ya wasishana Solya ambayo imefikia asilimia mbalimbali kuanzia 25 mpaka 90.

Aidha Serukamba alisema Halmashauri ilikwishapokea fedha kiasi cha Bilioni tatu ambazo zimetumika kujenga jengo la Utawala, mabweni matano yenye uwezo wa wanafunzi 120 kila bweni, majengo mawili yenye vyumba viwili vya madarasa vyoo, bwalo na  Maabara mbalimbali.

Alisema pamoja na changamoto nyingine zilizosababisha  ukwamo wa muendelezo wa Ujenzi wa shule hiyo changamoto nyingine ni  uzoefu mdogo wa kusimamia miradi mikubwa huku akieleza ugeni wa viongozi kuchangia kusuasua kwa Mradi huo.

Mwanzoni mwa Mwezi January mwaka huu Mkuu wa Mkoa Peter Serukamba alikutana na wananchi wa Wilaya ya Manyoni ambapo walitoa kero mbalimbali zikiwemo za upatikanaji wa maji, usalama wa raia na mali zao pamoja na migogoro ya ardhi ambayo yote aliisikiliza na kuitatua.

No comments:

Post a Comment