Sunday, February 05, 2023

Bilioni 7.562 kutumika kuchimba visima sita Mkoani Singida.

 

Wakala wa Usambazaji wa maji Safi na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wamesaini mikataba sita (6) yenye thamani ya Tsh. Bilion 7.56 ambayo inahusu uchimbaji wa visima katika Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Singida ili kupunguza tatizo la upatikanaji wa  maji mijini na Vijijini.

Akiongea kabla ya utoaji saini mikataba hiyo hafla iliyofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa Mkoa huo Mkuu wa Mkoa huo Peter Serukamba amewataka mameneja wa RUWASA wa Mkoa na Wilaya kusimamia zoezi hilo la uchimbaji visima kikamilifu ili kulinda thamani ya fedha zitakazotewa.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akisisitiza jambo wakati wa hafla ya usainishaji wa mikataba ya miradi ya maji mkoani Singida.

Aidha amewaagiza mameneja wa Wilaya na Mkoa wakiona Mradi wowote kati ya hiyo unasuasua  wahakikishe wanamchukulia hatua kali za kisheria Mkandarasi husika ili kutoa funzo kwa wengine na kuhakikisha thamani ya fedha inasimamiwa.

Hata hivyo amewataka wahandisi hao kusimamia kikamilifu maelekezo (Specification) ili pindi miradi ikamilike kwa ubora wake  na iwe na tija iliyokusudiwa.

"Hatutahitaji kazi inakamilika ndani ya miezi mitatu tunaambiwa maji hayatoki au tanki lina matatizo naomba tusimamie viwango "specifications" Serukamba.

RC Serukamba amesema endapo miradi hiyo ikikamilika katika viwango vilivyokusudiwa anaamini kwamba upatikanaji wa maji Vijijini utakuwa umefikia au umekaribia asilimia 85 na Mijini kwa asilimia 95.

"Tunataka tuache kuonge habari ya maji endepo miradi yetu ukikamilika tutaondoa tatizo la upatikanaji maji mijini na Vijiji" Serukamba

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida Martha Mlata amesema Serikali imeleta fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali hivyo ni jukumu la kila kiongozi kuhakikisha kwamba unatekelezwa kwa usahihi na kwa wakati.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida Martha Mlata akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM Mlata, ameeleza kwamba Mkoa wa Singida umeendelea kutekeleza miradi kwa viwango ambapo ameeleza kwamba kwenye miradi ya maji itawasaidia kumtua mama ndoo ya maji kichwani.

Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Mkoa wa Singida Mhandisi Lucas Said,  amesema miradi hiyo itatekelezwa na makampuni ya wazawa ambapo amesema kila Wilaya itakuwa na mradi mmoja.

Mhandisi Lucas Said  ameeleza kwamba miradi hiyo ikikamilika itaweza kuhudumia idadi ya watu wapatao 77,769 katika maeneo mbalimbali Mkoani hapo.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Singida Mhandisi Lucas Said, akizungumza wakati wa hafla hiyo.

No comments:

Post a Comment