Wakulima Kata ya Muhalala Wilaya ya Manyoni mkoani Singida wametakiwa kuongeza kasi ya ununuaji wa mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi zikiwemo alizeti, mtama na viazi wakati wakisubiri mvua ambazo zinatarajiwa kunyesha chini ya kiwango ili kuhakikisha wanapata mazao ya biashara na chakula.
Akiongea wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika leo 11 Januari 2022 katika Kata hiyo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge ametoa kauli hiyo wakati akikagua hali ya usambazaji wa mbegu za alizeti zenye ruzuku ya Serikali kwa wakulima wa Manyoni ambapo imeonekana Kata hiyo wakulima wamenunua kilo 245 tu kati ya kilo 2650 zilizopangwa katika Kata hiyo.
Aidha Dkt. Mahenge akawataka Maafisa Kilimo kuongeza uhamasishaji na elimu juu ya matumizi ya mbegu bora na umuhimu wa kilimo cha alizeti kwa mkoa huo ambapo wanatakiwa kununua mbegu hizo kwa gharama ya Sh. 3500 kwa kilo.
“Serikali imeweka ruzuku kwenye mbegu za alizeti badala ya kuuzwa shilingi 15000 watanunua kwa sh. 3500 hivyo kila mkulima anunue mbegu wakati akisubiri mvua”. Alisema RC Mahenge
RC Mahenge akafafanua kwamba wataalamu wa hali ya hewa wamebainisha kwamba kiwango cha mvua kitakachopatikana kwa mkoa wa Singida ni cha wastani ambacho kitafaa baadhi yakiwemo alizeti na mtama.
Dkt. Mahenge akawakumbusha wananchi wote wa Mkoa huo kupitia mkutano wake na wananchi wa Muhalala kutunza na kutumia chakula vizuri kwa kuwa hali ya hewa inaonesha kwamba msimu ujao kutakuwa na upungufu wa mazao ya chakula kutokana na upungufu wa mvua msimu huu.
“Endapo tukilima alizeti, mtama na viazi mazao haya kwa kuwa yanachukua muda mfupi kukomaa na yanahitaji mvua kidogo, yatatusaidia kupata chakula na fedha, kwa kufanya hivyo mkoa wa Singida hatutakuwa kwenye hatari ya upungufu wa chakula”. Alikaririwa RC Mahenge.
Naye Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya uchumi na uzalishaji mkoani hapa Bw. Beatus Choaji amesema Wilaya ya Manyoni imepata jumla ya tani 48 za mbegu za alizeti ambapo tani 40 tayari zimesambazwa katika Kata mbalimbali.
Aidha amebainisha kwamba mbegu hizo zinatolewa kwa mkopo kwa wakulima ambapo watakuja kulipa baada ya mavuno japo wenye uwezo wa kununua watapatiwa huduma hiyo alisisitiza Bwana Choaji.
Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Wilaya ya Manyoni Fadhili Chimsala amesema bado wanaendelea kuhamasisha wakulima katika kata mbalimbali wilayani hapo ili kununua mbegu za alizeti japo bado wakulima wengi walikuwa hawajajitokeza kwa sababua walihofia mvua ya msimu huu kuwa kidogo.
Bwana Chimsala akaendelea kusema kwamba Wilaya kwa kushirikiana na wataalamu wa Wizara ya Kilimo wameendelea kutoa mafunzo kwa wananchi juu ya namna bora ya kutunza na kuhifadhi chakula ili kuwasaidia wakati wa mahitaji.
Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Rahabu Mwagisa akizungumza wakati wa mkutano (kushoto) ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge.
No comments:
Post a Comment