Monday, January 10, 2022

Dkt. Mahenge asisitiza Majadiliano katika kutatua Migorgoro ya Wakulima na Wafugaji.

 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge leo amekutana na Viongozi wa wafugaji kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Itigi lengo likiwa ni kutafuta suluhisho la mgogoro wa ardhi inayo endele katika vijiji mbalimbali wilayani hapo.

Akiongea wakiwa ofisini kwake RC Mahenge amewataka Viongozi hao kutumia njia ya majadiliano  kutatua migogoro baina yao na wakulima badala ya matumizi ya nguvu ambapo amewataka  kuyapitia makubaliano ya awali na kuona kama  yameathiriwa namna gani na ongezeko la watu, mifugo au athari za tabia ya nchi kabla ya kufanya maamuzi.

“Hivi karibuni Serikali imetatua migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kutoa maeneo ya hifadhi na kuyagawa kwa wananchi, wafugaji na wakulima kwa kuwa idadi ya watu na mifugo vimeongezeka, hivyo katika kujadili changamoto hizo tutalazimika pia kuangalia matokeo hayo”. Alisema RC Mahenge

Amesema japo Serikali ilishaweka mipango ya matumizi bora ya ardhi lakini endapo idadi ya watu au mifugo itaongezeka bado kutakuwa na fursa ya kukaa na kuangalia namna ya kushughulika na tatizo husika.

Awali akielezea lengo la ujio wao Mwenyekiti wa chama cha wafugaji Bwana Elifasi Lwanji amevitaja  vijiji ambavyo maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo yamevamiwa na  wakulima ambayo ni Sanjaranda Doroto na Damwelo katika Hamashauri ya Wilaya ya Itigi.

Aidha mwenyekiti huyo amemshukuru  Mkuu wa Mkoa kukubali kuyatembelea maeneo yaliyoathirika  ili kusikiza malalamiko yao na ikiwezekana kuchukua hatua ili kuepusha migogoro ambayo ingeweza kutokea.

Naye Joramu Mathayo ambaye ni Katibu wa chama cha wafugaji Halmashauri ya Itigi amesema walishafanya mikutano mikuu ya kijiji na maamuzi yalishatolewa lakini wakulima wanaonekana kutokuwa tayari kufuata maamuzi sahihi ya mikutano hiyo.

Amebainisha kwamba pamoja na kwamba maeneo hayo yalishapangiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi na maamuzi ya Mahakama yaliwataka wakulima hao kuondoka lakini hawakufanya hivyo jambao ambalo tunahisi kwamba kuna kikwazo baina yao alimalizia Bwana Joramu.

Akitolea ufafanuzi juu ya migogoro katika vijiji hivyo  Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya uchumi  na uzalishaji mkoa wa Singida  Beatus Choaji amesema Serikali kupitia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ilishafika katika vijiji hivyo na kutoa elimu kwa wananchi hao japo inaonekana upande mmoja uliendelea kubaki na maamuzi yake.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa ameahidi kutembelea vijiji hivyo hivi karibuni ambapo atafanya mkutano na wahusika wote  ili kuweza kutatua changamoto zinazoendelea.

No comments:

Post a Comment