Jumla ya wanafunzi 28,072 waliofaulu mitihani ya darasa la saba kwa mwaka 2021 mkoani Singida watapata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022 kutokana na uwepo wa vyumba vya madarasa zaidi ya 330 vilivyojengwa kwa fedha za Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa katika Halmashauri mbalimbali mkoani hapo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya vyumba 662 vya madarasa na mabweni mawili iliyofanyika kimkoa Disemba 31, 2021 katika shule ya Sekondari Isuna, wilayani Ikungi.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Binilith Mahenge wakati akikabidhiwa vyumba vya madarasa katika mkutano uliofanyika Kata ya Isuna wilayani Ikungi Disemba 31, 2021.
Akiwa katika mkutano huo RC Mahenge akamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa jumla ya Sh.Bilioni 13.4 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu mkoani hapa.
Dkt. Mahenge amesema mkoa ulikuwa na uwezo wa kupeleka wanafuzi wa Sekondari 11,520 pekee kwa wakati mmoja lakini baada ya fedha hizo jumla ya madarasa 330 yamejengwa na wanafunzi 16,500 wa Sekondari wataanza shule mapema January 2022.
Aidha RC Mahenge akabainisha kwamba ujenzi wa vyumba vya madarasa uliofanyika katika wilaya zote mkoani hapo zimetoa fursa kwa vijana na wakina mama kupata ajira kwa kushiriki kazi mbalimbali pamoja na kufanya biashara ya chakula kwa ajili ya mafundi na vibarua mbalimbali.
Muonekano wa moja ya vyumba vya madarasa yaliyojengwa mkoani Singida kupitia fedha za Mandeleo kwa Ustawi wa Taifa.
Akimalizia hotuba yake Mahenge amewataka Wakurugenzi kuanza maandalizi ya kuendelea na ujenzi wa vyumba mbalimbali kwa kutumia fedha za ndani badala ya kusubiri msaada kutoka ngazi za juu.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida Mwl. Dorothy Mwaluko akimkaribisha Mkuu wa Mkoa ameeleza kwamba fedha zilizopokelewa kwa upande wa elimu zilikusudiwa kujenga vyumba vya madarasa 662 na mambweni mawili (2) ili kuweza kupokea wanafunzi wote kwa wakati mmoja.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko akizungumza wakati wa hafla hiyo.
RAS Mwaluko amesema ubunifu mkubwa umefanyika katika ujenzi wa madarasa hayo ambapo tayari jumla ya ofisi 63 za walimu nazo zimekamilika ujenzi ambao haukuwepo kwenye mahesabu ya awali.
Amesema miradi hiyo imetoa funzo kubwa kwa watendaji kwa kuwa wameweza kutumia njia mbalimbali za kufanya manunuzi ikiwemo manunuzi ya pamoja (balk procurement) pamoja na changamoto zake ambapo amewataka wasimamisizi wa miradi mbalimbali kuchanganua changamoto zinazojitokeza ili kufanya maamuzi sahihi wakati wa ununuzi wa vifaa wakati mwingine.
Awali akitoa taarifa ya vyumba vya madarasa DC wa Ikungi Jerry Muro amesema walipokea Sh. Bilioni 2.64 za Miradi ya Maendeleo ya Taifa lengo likiwa ni kujenga vyumba vya madara 132 ambavyo vimetekelezwa kwa ushirikiano mkubwa wa viongozi mbalimbali pamoja na wananchi wa Wilaya hiyo.
Dc Jerry Muro amefafanua kwamba katika fedha hizo jumla ya Sh. Bilioni 1.3 zilitumika kujenga vyumba 67 katika shule za sekondari 28 na Sh.Bilioni 1.3 zilitumika kujenga madara 65 katika shule za msingi 16 ambapo jumla ya vyumba 132 vimekabidhiwa.
Aidha Jerry amewashukuru wananchi kwa ushirikiano wao mkubwa katika kufanikisha zoezi hilo kwa kujitolea nguvu kazi hasa kwa kuleta mchanga, maji na kusomba vifusi jambo ambalo lilisaidia kukamilisha jukumu hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sindida Mhandisi Paskas Muragili akiendelea kutoa shukrani kwa Serikali amebainisha kwamba jumla ya wanafunzi 3,976 wanatoka Manispaa ya Singida watafaidika na ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa.
Hata hivyo Mhandisi Muragili akaongeza kwamba wilaya nzima ya Singida ina jumla ya wanafunzi 9,737 watakao nufaika na ujenzi wa madarasa wakiwemo 5791 kutoka Halmashauri za Singida vijijini.
MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro akitoa taarifa ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika wilaya hiyo wakati wa hafla hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo akitoa taarifa ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika wilaya hiyo wakati wa hafla hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda akitoa taarifa ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika wilaya hiyo wakati wa hafla hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Rahabu Mwagisa akisoma taarifa ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika wilaya hiyo wakati wa hafla.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ikungi Mika Likapakapa akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida Alhaji Juma Kilimba kwenye hafla hiyo.
Hafla ikiendelea
Muonekano wa ndani ya darasa lililojengwa kwa fedha za Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa
Viongozi wa Serikali ya Mkoa wa Singida wakiwa ndani ya moja ya darasa wakimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo za ujenzi wa madarasa kwa shule za msingi na sekondari ambapo zimesaidia kupunguza kero waliyokuwa wanaipata wananchi kwa kutozwa michango mbalimbali kwa ajili ya kukamilisha maboma na utengenezaji wa madawati hasa kipindi hiki ambacho shule zinakaribia kufunguliwa.
No comments:
Post a Comment