Friday, February 03, 2023

Serukamba amaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa miaka zaidi ya 30.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amewataka wananchi wa Mkoa huo kufuata taratibu za upimaji wa ardhi na kuzimiliki kihalali ili kupunguza migogoro ya ardhi katika jamii.

Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 3/02/2023 wakati akitatua mgogoro wa mpaka uliodumu kwa miaka 30 katika eneo la ukubwa wa ekari 132 lililopo katika kijiji cha Kititimo kata ya Mungu maji katika Manispaa ya Singida.

Eneo hilo ambalo limetajwa kumilikiwa kisheria na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) tangu mwaka 1945 lilivamiwa na wananchi ambao wakijenga na wangine kufanya shughuli za kilimo.

Hata hivyo RC Serukamba amewatoa wasiwasi wananchi wenye makazi katika eneo hilo kwa kipindi kisichopungua miaka 12 kwamba hataondolewa katika maeneo yao na kuagiza Halmashauri kuwapimia ili waweze kumilikishwa kihalali huku akieleza kwamba mashamba yote yatabaki katika umiliki wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Amewataka wananchi kujenga tabia ya kumiliki maeneo (ardhi) kisheria badala ya kufanya uvamizi jambo ambalo litakuwa likiwasababishia hasara kila mara.

"Tuache tabia ya kuvamia maeneo ya watu itakusababishia hasara na ukiwa na eneo lako hakikisha linapimwa ili ulimiliki kisheria" Serukamba.

Aidha Serukamba ametoa onyo kali kwa wananchi wa Kititimo kwamba isije ikatokea mtu yeyote akang'oa "Bikoni" zilizowekwa kwa kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA


Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (kushoto) akimsikiliza moja ya Mzee wa eneo lililokuwa na mgogoro.




Zoezi la upimaji na uwekaji bikoni likiendelea katika eneo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akisisitiza jambo kwa wakazi wanaolizunguka eneo hilo lililokuwa na mgogoro.


No comments:

Post a Comment