Tuesday, July 05, 2022

RC Mahenge awataka Viongozi Mkoani Singida kutatua Kero za wananchi

MKUU wa Mkoa wa Singida, Dk.Binilith Mahenge, amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na watendaji katika wilaya zote za mkoa huu kufanya ziara kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi badala ya kusubiri viongozi wa Serikali ya mkoa ndio wazitatue changamoto za wananchi.

Ametoa agizo hilo wakati wa kikao maalum cha kufanya majumuisho ya ziara yake aliyoifanya hivi karibuni katika wilaya zote za mkoa huu kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi.

Dk.Mahenge alisema serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo lakini wananchi hawajui kinachoendelea kwasababu viongozi ambao wanapaswa kuwaeleza hawafanyi hivyo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge akizungumza wakati wa Mkutano huo.

"Ni muhimu mno kufanya mikutano ya wananchi kusikiliza kero zao, wahamasisheni madiwani, makatibu tarafa wafanye ziara, mkoa wetu mwaka wa fedha uliopita tulipata Sh.230 bilioni ni wajibu wetu kama viongozi kuzisimamia ili zilete tija katika maendeleo," alisema.

Dk.Mahenge alisema wakuu wa wilaya wanajitahidi sana kufanya ziara na kusikiliza kero za wananchi lakini changamoto ipo kwa watendaji wengine wa serikali ambao hawafanyi hivyo na hivyo kusababisha kuibuka kwa kero nyingi ambazo kama ziara zingekuwa zinafanyika hali hiyo isingejitokeza.

Aliongeza kuwa katika baadhi ya maeneo wananchi wamekuwa wakilalamika kutoshirikishwa kwenye mipango mbalimbali ya maendeleo hususani baadhi ya wenyeviti wa serikali za vijiji ambao ndio wamekuwa na tabia hiyo.

"Baadhi ya wenyeviti wa vijiji wamekuwa kama miungu watu hawatowi fursa ya kusikiliza wananchi, RAS (Katibu Tawala Mkoa) tufanye uchunguzi na tuchukue hatua kwa kuzingatia sheria na taratibu za serikali," alisema Dk.Mahenge.

Aidha, Dk.Mahenge aliagiza wakuu wa wilaya kwa kushirikiana na wataalam wa ardhi kufuatilia migogoro yote ya ardhi na kuipatia ufumbuzi na kuiweka kwenye 'data base'.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa huo kuwa yote aliyoyaagiza atayafanyia kazi kwa kushirikiana na Watendaji wa Halmashauri za Mkoa.

Mkutano ukiendelea

MWISHO

No comments:

Post a Comment