Wednesday, June 29, 2022

Tutapima udongo kabla ya kusambaza mbegu za alizeti RC Mahenge

 

Serikali imejipanga kupima na kutambua  Hali ya udogo kabla ya kusambaza mbegu za alizeti kwa wakulima wa Mkoa wa Singida ili kuondoa  changamoto iliyojitokeza katika msimu huu wa kilimo ambapo kwa bàadhi ya maeneo hazikuweza kutoa mazao yaliyokusudiwa.

Lengo la kupima udongo wa maeneo hayo ni kutambua aina ya mazao au mbegu zinazoweza kustawi  kwa kuwa imebainika  kwamba bàadhi ya mbegu za alizeti zimekuwa zikistawi zaidi katika bàadhi ya maeneo huku maeneo mengine  zikishindwa kustawi vizuri.

Akiongea wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Kitukutu kata ya Kiomboi wilaya ya Iramba alipokuwa akisikiliza na kutatua Kero za Wananchi Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge amebainisha kwamba Serikali inaendelea na mpango wa kupima ardhi ili kubaini aina ya mazao yanayoweza kustawi pamoja na aina ya mbolea itakayopendekezwa kutumika maeneo husika.

 Pamoja na changamoto ilijitokeza kwa wakulima wa alizeti katika bàadhi ya maeneo ambapo mbegu aina ya  standard kushindwa kustawi vizuri RC Mahenge akawaeleza wananchi kwamba  Serikali iligawa mbegu za alizeti kwa wananchi zenye thamani ya Tsh. Bilion tatu lengo likiwa ni kuondoa umaskini kwa wananchi kwa kupitia kilimo lakini mbegu hazikuweza kustawi vizuri kama malengo yalivyokuwa.

Amesema Serikali inampango wa kupima udongo katika maeneo mbalimbali Mkoani hapo ili  kubaini aina ya udongo na aina ya mbegu zinazotakiwa kustawishwa ili kuondokana na changamoto ya kupanda mbegu ambazo hazitaweza kutoa mafanikio.

Akijibu swali la mwanakijiji Elizabeth Shalua ambapo alitaka kujua mpango wa Serikali kuhusu mbegu hizo za alizeti ambazo ulikuwa ni mkopo kutoka Wizara ya Kilimo ambao waliotakiwa kurejesha wakati wa mavuno  na kwa bahati mbaya wameshindwa kuvuna kutokana na mbegu hiyo kutoa Mashuke kidogo RC Mahenge akabainisha kwamba kwa sasa Serikali haitadai kwa kuwa wananchi tayari wameingia hasara.

Naye Emanueli Mitundu kutoka Kijiji cha Misigiri akatumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kupunguza bei ya pembejeo ikiwemo mbolea ambayo imekuwa juu kiasi cha wakulima kushindwa kununua hivyo kuchangia kupata mazao hafifu.

Ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa imeendelea katika Kijiji cha Misigiri ambapo aliendelea kutatua Kero za Wananchi kuhusu upatikanaji wa maji, Umeme na Barabara huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali katika kutatua Kero zinazowakabili.

Aidha ziara hiyo ya kusikiliza na kutatua Kero za Wananchi itaendelea katika Wilaya ya Mkalama katika Kijiji cha Iguguno katika Mkutano wa hadhara utakofanyika uwanja wa Ofisi ya Kijiji cha Iguguno kuanzia saa tano asubuhi.

Mwisho


No comments:

Post a Comment