Moja ya eneo linalotumika katika shughuli za uchimbaji
Wawekezaji mkoani Singida wametakiwa kushirikiana na
Halmashauri za Wilaya wakati wa kuanzisha miradi ya Maendeleo ya Kijamii (Community
Socially Responsibility – CSR) ili kukubaliana aina za miradi na namna
itakavyotekelezwa lengo likiwa ni kuepuka matumizi makubwa ya fedha kwa kazi
ambazo zingetumia fedha kidogo.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Binilith
Satano Mahenge leo January 26, 2022 alipotembelea machimbo ya madini ya dhahabu
yanayochimbwa na kampuni ya Shanta Gold iliyopo kijiji cha Mang’onyi wilayani
Ikungi ambapo alieleza kwamba miradi yote inayoanzishwa na wawekezaji ipitie
katika Halmashauri za Wilaya ambazo zinafahamu mahitaji ya wahusika na gharama halisi za ujenzi katika maeneo hayo.
Akitolea mfano kwa madarasa yalikamilika hivi karibuni
kupitia fedha za uviko 19 RC Mahenge amesema kila darasa liligharimu kiasi cha
shilingi milioni 20, ikilinganishwa na madarasa yaliyojengwa na Shanta Gold
ambayo yamegharimu Tsh.milioni 28 kwa kila darasa.
“Kama mradi huu mngeshirikisha Halmashauri kwa kiasi kikubwa
mngetumia Force Account na mgepata wakandarasi wa bei ndogo na fedha zingebaki
zikafanya maendeleo mengine katika jamii. Niwashauri mshirikiane ipasavyo na
Halmashauri kupanga aina ya miradi mnayotaka kuipeleka kwa jamii”, alisema Rc
Mahenge.
Hata hivyo RC Mahenge akaipongeza Kampuni hiyo ya Shanta Gold
kwa kutumia zaidi ya Milioni 190 kwa kupeleka huduma kwa jamii ikiwemo ujenzi
wa vyumba viwili vya madarasa na uchimbaji wa visima vya maji huduma ambazo
zinafaidisha vijiji vya Mang’onyi, Sambaru, Mlumbi, Tupendane na Mwau.
Aidha, Dkt. Mahenge akaitaka jamii inayozunguka mgodi huo
kutumia fursa na kuwa wabunifu kwa kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo ufugaji
wa kuku na mama lishe pamoja na kuomba ajira katika kampuni hiyo kwa kuwa kadri
mradi unavyokuwa ndivyo mahitaji yatakavyoongezeka.
Awali akitoa taairifa ya mgodi Meneja wa Mradi huo Kundael
Mtiro amesema mpaka kufikia sasa mradi ulitakiwa kufikia asilimia 46.14 katika
utekelezaji wake lakini kwa sababu ambazo zimekuwa nje ya uwezo mpaka sasa
utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 43.62 .
Hata hivyo Mtiro akaendelea
kufafanua kwamba mpaka June, 2022 mradi utakuwa unakamilisha robo ya nne ya mwaka ambapo wanategemea
kwamba utakuwa umekamilika kwa kuwa tayari washasimika mabomba katika maeno
yote yanayohusika pamoja na uchimbaji wa visima, ujenzi wa ofisi na makazi
umekamilika kwa asiliami 80.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro amesema mgodi huo
utainua uchumi wa Singida na taifa kwa ujumla ambapo utasisimua sekta nyingine za
elimu barabara, zahanati na wananchi kupata ajira.
Amesema Wilaya imeendelea kusimamia hali ya usalama katika
eneo la mradi na imehakikisha wanachi wote waliokuwa wanastahili kupata fidia
zao wamelipwa kwa wakati.
MATUKIO MBALIMBALI WAKATI WA ZIARA
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge akizungumza mara baada ya kuwasili katika moja ya eneo linalotumika katika shughuli za uchimbaji
No comments:
Post a Comment