Mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Singida Dkt Mohamed Mbalazi
akitoa mada katika mkutano ulijadili uboreshaji wa ushirikiano baina ya
serikali na wadau wa sekta binafsi zinazotoa huduma ya Afya Mkoani Singida.
Afisa Lishe Mkoa wa Singia Teda Sinde akifafanua jambo
katika mkutano ulijadili uboreshaji wa ushirikiano baina ya serikali na wadau
wa sekta binafsi zinazotoa huduma ya Afya Mkoani Singida, Kushoto kwake ni Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Singida Jadili Mhanginonya.
Mratibu wa
Kifua Kikuu na Ukoma Mkoa wa Singida Dkt Evans Mlay (wa kwanza kushoto)
akipitia dondoo, kabla ya kuwasilisha mada iliyoonyesha mchango mkubwa wa wadau wa
Sekta ya Afya katika mapambano dhidi ya Kifua Kikuu Singida, Kulia kwake ni Afisa
Mradi wa AMREF Mkoa wa Singida Donathapeace Kayoza.
Wadau mbalimbali wa sekta binafsi wameweza kuongeza
nguvu katika kuboresha sekta ya Afya Mkoani Singida kutokana na ushirikiano
mzuri ulipo baina yao na serikali.
Hayo yamebainishwa katika mkutano maalumu wa siku mbili
uliohitimishwa jana Mjini Singida, ambapo viongozi wa serikali, taasisi na
mashirika 15 yanayotoa huduma za Afya na Ustawi wa jamii Mkoani hapa wamejadiliana
namna ya kuboresha ushirikiano baina yao.
Mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Singida Dkt Mohamed Mbalazi
amesema katika mapambano dhidi ya Ukimwi na Virusi vya Ukimwi (VVU) Mkoani
hapa, Sekta binafsi zimekuwa na mchango mkubwa.
Dkt Mbalazi amesema wadau hao wameweza kutoa dawa za
kupunguza makali ya VVU, tiba lishe, mafunzo kwa watoa huduma wa afya,
ufuatiliaji wa watumiaji wa dawa za VVU pamoja na kuandaa takwimu jambo ambalo
limeboresha mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi.
“Sisi kama watendaji wa serikali tunathamini na
kutambua mchango wa wadau wa sekta afya kwakuwa ni nguzo muhimu sana, mfano
wadau wetu shirika la EGPAF, wametenga bilioni 1.6 kwa ajili ya mapambano dhidi
ya Ukimwi na maambukizi ya VVU Mkoani Singida”, amesema na kuongeza kuwa,
“Fedha hizo zitaongea nguvu pale ambapo kuna
changamoto au bajeti inakuwa haitoshelezi, lakini pia tunaendelea kutoa wito
kwa wadau wengine waendelee kuongea nguvu na wigo wa ushirikiano kwakuwa lengo
letu ni moja yaani kumsaidia mwananchi apate huduma bora za afya”, amesisitiza
Dkt Mbalazi.
Naye Afisa Lishe Mkoa wa Singida Teda Sinde amesema
wadau wamekuwa watekelezaji wazuri wa masuala ya Lishe Mkoani hapa hasa kwa ngazi
ya jamii hivyo ushirikiano kati yao umekuwa wa manufaa makubwa.
Teda amesema mkutano huo wa wadau umewawezesha
watendaji na viongozi wa serikali kuelewa kwa upana zaidi kazi wanazofanya
wadau pamoja na changamoto wanazopitia ili waweze kusaidiana katika kuboresha
hali ya Lishe Mkoani hapa.
“Mkutano huu umeongeza na kuboresha ushirikiano baina
yetu na wadau wetu ambao wengi wao wanatoa chakula lishe na elimu ya lishe kwa
akina mama wajawazito, watoto wenye umri wa miezi sita mpaka 59 na akina mama
wanaonyonyesha watoto chini ya miezi sita”, ameeleza Teda.
Ameongeza kuwa mkutano huo umeweza kusaidia katika
kupanga mikakati ya utoaji huduma ili kuepusha wadau wanaotoa huduma ya aina
moja kutoelekeza nguvu katika maeneo yanayofanana au ambayo hayana uhitaji
mkubwa kuliko maeneo mengine.
Akifungua Mkutano huo Mwakilishi wa
Kaimu Katibu Tawala Mkoa, Cosmas Sikali aliwataka wadau kujadili sera, sheria,
kanuni, maeneo ya kipaumbele katika miradi mbalimbali, mafanikio na changamoto
katika utekelezaji wa mipango mikakati inayosisitiza ushirikiano kati ya Sekta
ya Umma na binafsi.
Sikali amesema endapo nguvu hizi kwa
pamoja zitaunganishwa na kuratibiwa vizuri kwa kiasi kikubwa changamoto
zilizopo katika sekta ya afya na ustawi wa jamii pamoja na maradhi kwa wananchi
yataweza kupungua.
Ameongeza
kuwa serikali peke yake haitaweza kufikia malengo ya kupunguza vifo vya
watoto, akina mama wajawazito na kuweza kudhibiti magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza, pamoja na kuboresha afya ya mazingira na kupata maji safi na salama bila kushirikiana na Sekta binafsi.
Dkt
Manyatta amesema mkutano huo umeweka malengo na maazimio ya pamoja na wadau wa
sekta binafsi ili kuimarisha sekta ya afya na ustawi wa jamii Mkoani Singida.
Mwakilishi wa Kaimu Katibu Tawala
Mkoa, Cosmas Sikali akizungumza na wadau wa sekta binafsi zinazotoa huduma
katika Mkoa wa Singida.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt
Salum Manyatta akisikiliza kwa makini maoni na michango mbalimbali ya wadau
ambao ni taasisi na mashirika binafsi yanayotoa huduma za Afya Mkoani Singida.
Meneja Mradi wa EGPAF Kanda ya Kati
Dkt Joseph Obedi akiandika baadhi ya mapendekezo ya kuboresha ushirikiano kati
ya sekta binafsi na serikali katika uboreshaji wa huduma za Afya Mkoa wa
Singida.
No comments:
Post a Comment