Thursday, September 28, 2017

HALMASHAURI ZIONGEZE MABWAWA KWA AJILI YA KILIMO CHA UMWAGILIAJI; NAIBU WAZIRI KAMWELWE.

Naibu Waziri Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack A. Kamwelwe na Mkuu wa Mkoa wa Singida wakisoma kwa umakini taarifa ya Sekta ya maji Mkoa wa Singida wakati wa kikao na wakuu wa idara mbalimbali.
Naibu Waziri Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack A. Kamwelwe akisikiliza taarifa ya mradi wa maji wa Ughandi kutoka kwa Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Edward Kisalu.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Singida Patrick Girigo Kasango na Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Singida Eva Mosha wakimsikiliza Naibu Waziri Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack A. Kamwelwe.
 
Naibu Waziri Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack A. Kamwelwe amezitaka halmashauri za Mkoa wa Singida kuongeza ujenzi wa mabwawa, utakaosaidia kilimo cha umwagiliaji ili kuzalisha chakula cha kutosha na kwa ajili ya makao makuu ya nchi, Dodoma.

Mhandisi Kamwelwe ametoa maelekezo hayo wakati wa mkutano uliojumuisha wakuu wa idara zote pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Singida ili kujadili hali ya Sekta ya Maji kabla ya hajaendelea na ziara yake katika halmashauri za Mkoani hapa.

Amesema ardhi ya Singida pamoja na kiwango cha mvua cha milimita 500 mpaka 800 kwa mwaka vinatosha kuzalisha chakula kwa ajili ya matumizi ya mkoa lakini ujenzi wa mabwawa utaongeza uzalishaji wa chakula hasa kwa lengo la kulisha mkoa wa Dodoma.

“Mkuu wa Mkoa wa Singida una malengo makubwa na mazuri kwa mkoa huu, mpango wako wa kuifanya Singida iilishe Dodoma ni mzuri na utafanikiwa hasa mkiongeza bidii katika uzalishaji na kuweka kipaumbele katika kilimo cha umwagiliaji”, amesema Mhandisi Kamwelwe.

Ameongeza kuwa Singida inapata mvua za wastani lakini imekuwa ikizalisha kwa wingi mazao ambayo yamekuwa yakitumika katika mikoa yote nchini kwa mfano alizeti, viazi vitamu, vitunguu na asali ambapo mazao hayo yamekuwa yakipendwa kutokana na ubora wake.

Mhandisi Kamwelwe ameongeza kuwa hali ya upatikanaji wa maji kwa Mkoa wa Singida bado inatakiwa kuboreshwa zaidi kutokana na kuwa kila mwaka serikali imekuwa ikitenga fedha nyingi lakini asilimia ya upatikanaji wa maji haiongezeki kwa kasi inayotakiwa.

Aidha amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Singida kusimamia matumizi ya fedha za serikali zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maji ili ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa na kwa ubora mkubwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amesema kuwa Singida sio kame kwakuwa hakuna mazao yanayoweza kumea katika ukame isipokuwa Singida imejikita katika mazao yanayotumia maji kwa ufanisi.

Dkt Nchimbi amesema Singida inazalisha mazao ya mahindi, alizeti, vitunguu, viazi vitamu na mazao mengine kwa wingi kutokanana na kuwa mvua zinazonyesha zinatosheleza kustawisha mazao hayo.

Ameongeza kwa kuwataka wakuu wa idara zote kusimamia matumizi bora ya fedha za serikali zinazotolewa kwa ajili ya maji kwakuwa suala la maji ni la kila mmoja na sio kuwategemea watumishi wa idara hiyo pekee katika kusimamia fedha na miundominu ya maji.

Dkt Nchimbi amesema Mkoa unahamasisha uchimbaji wa mabwawa kwa halmashauri, taasisi na hata makundi mengine kwakuwa mabwawa hayo yatasaidia kuinua kilimo cha umwagiliaji Mkoani Singida pamoja na kukuza uchumi.

Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Singida Buhacha Kichinda amesema hali ya upatikanaji wa maji kwa Mjini ni asilimia 50.6 huku vijijini ikiwa ni asilimia 44 na kuongeza kuwa wastani huo ni mdogo kwakuwa unarudisha nyuma jitihada za kuinua uchumi.

Kichinda amesema Mkoa umejipanga kushirikisha wadau zaidi ili kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi ya maji ya visima virefu pamoja na ujenzi wa mabwawa pamoja na kusimamia fedha zote za serikali zinazotolewa kwa ajili ya sekta ya maji zinatumika ipasavyo.

Amesema ili kuhakikisha mvua zinaendelea kunyesha vizuri pamoja na kutunza vyanzo vya maji, mkoa umeweka mkakati wa “ Achia shoka Kamata Mzinga” ili kuwahamasisha wachoma mikaa waache kukata miti bali wajikite katika kutundika mizinga itakayotunza mazingira.


Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Singida Buhacha Baltazar Kichinda akisoma taarifa ya sekta ya Maji kwa Katibu Tawala Mkoa wa Singida Buhacha Kichinda.

Naibu Waziri Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack A. Kamwelwe akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ughandi A halmashauri ya Wilaya ya Singida alipotembelea eneo la mradi wa maji kijijini hapo.

No comments:

Post a Comment