Mkuu wa Mkoa Singida Dkt. Parseko V. Kone akizungumza na waandishi wa habari juu ya mbio za mwenge wa uhuru Mkoani Singida kulia kwake ni katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan.
Mkuu wa Mkoa wa Singida
Dkt.Parseko V. Kone amewataka wananchi
Mkoani humo kushirikiana katika kusimamia
miradi itakayowekewa mawe ya msingi na Mwenge wa Uhuru ili thamani halisi ya fedha zitakazotumika
iweze kupatikana na miradi hiyo kukamilika kwa wakati.
Dkt. Kone ametoa wito
huo leo asubuhi katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakati akiongea na
waandishi wa habari juu ya mbio za mwenge wa uhuru kwa mwaka 2014 Mkoani
Singida zitakazoanza rasmi kesho asubuhi.
Amesema Mwenge wa Uhuru
unatarajiwa kupokelewa katika kijiji cha Rungwa Tarafa ya Itigi Wilaya ya
Manyoni ukitokea Mkoani Mbeya na utakimbizwa katika halmashauri sita za Mkoa wa
Singida kisha kukabidhiwa Mkoa wa Dodoma, Wilaya ya Chemba kijiji cha
Kinyamshindo tarehe 10 Juni 2014.
Dkt. Kone ameongeza
kuwa Mwenge wa uhuru utazindua, kuweka mawe ya msingi na kutembelea miradi 60
yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 5.9 katika sekta za afya, elimu,
maji, barabara, kilimo,ufugaji, ushirika, misitu na sekta binafsi.
Wakimbiza Mwenge Mkoa wa Singida wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko V. Kone muda mfupi kabla ya kuelekea kijiji cha Rungwa tayari kwa kuupokea Mwenge wa Uhuru Mkoani Singida.
Aidha amewasihi
wananchi kufika katika maeneo ambapo salamu za Mwenge zitatolewa ili kupata na
kuuzingatia ujumbe huo.
Dkt. Kone ameongeza
kuwa moja ya ujumbe wa mwenge ni suala la kukamilisha mchakato wa katiba mpya
huku akisisitiza wananchi kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kushiriki katika
mchakato huo bila ya kuathiri umoja, amani na utulivu wa nchi yetu.
Amesema mbio za Mwenge
wa uhuru kwa mwaka 2014 zimebeba ujumbe usemao “Katiba ni sheria kuu ya Nchi” huku kauli mbiu ikiwa ni “Jitokeze
kupiga kura ya maoni tupate Katiba Mpya”
Pia ujumbe huo
utaambatana na kauli za uhamasishaji jamii kupitia ujumbe wa kudumu wa Mwenge
kuhusu mapambano dhidi ya Ukimwi yenye kauli mbiu isemayo “Maambukizi mapya,
unyanyapaa na vifo vitokanavyo na Ukimwi sifuri”.
Mapambano dhidi ya
rushwa yatahamasishwa kwa kauli mbiu isemayo “Palipo na rushwa hakuna maendeleo”
wakati huohuo kauli mbiu ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya itakuwa ni “Furahia
afya yako sio dawa za kulevya”.
Wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Singida (wa kwanza ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Geofrey Kamwela) wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko V.
Kone muda mfupi kabla ya kuelekea kijiji cha Rungwa tayari kwa kuupokea Mwenge
wa Uhuru Mkoani Singida.
No comments:
Post a Comment