
Na Glory Kimaro
Katika kuimarisha utalii na kuvutia uwekezaji, Mkoa wa Singida unatarajia kuandaa Tamasha la Utalii na Utamaduni kuanzia Desemba 15 hadi 19, 2026, likilenga kutangaza vivutio vya utalii, fursa za biashara na uwekezaji pamoja na kuongeza ajira kwa wananchi, hususan vijana na wanawake.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika Regency Hotel, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, amesema tamasha hilo ni mwendelezo wa juhudi za Serikali za kutangaza utalii nchini, zilizopata msukumo mkubwa kupitia filamu ya The Royal Tour iliyoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Dendego amesema tamasha hilo litahusisha maonesho ya utalii kwa siku zote tano kuanzia Desemba 15 hadi 19, Tamasha la Utamaduni litakalofanyika Desemba 15 hadi 17 na kuhitimishwa na Kuku Choma Festival, Kongamano la Uwekezaji Desemba 16, Sekenke Marathon Desemba 17 pamoja na mashindano ya magari Desemba 18, huku kilele cha tamasha kikiwa Desemba 19, 2026.
Amesisitiza kuwa utalii si shughuli ya kutembelea vivutio na kujiburudisha pekee, bali ni sekta yenye fursa pana za uwekezaji, biashara na ajira, hivyo amewaalika wawekezaji, wafanyabiashara na wananchi kutoka maeneo mbalimbali kushiriki. Ameeleza kuwa Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, Kampuni ya Kilimanjaro Sports Promotion na wadau wengine imejipanga kupokea wageni na washiriki hao, kwa kuhakikisha usalama na huduma bora zinapatikana.
“Tunatarajia kuongeza ajira hasa kwa vijana na wanawake, kutangaza mkoa na fursa zake za utalii na uwekezaji, kuchangia huduma za afya, kuvutia na kukuza uwekezaji, kuwaleta watu pamoja na kukuza mshikamano,” amesema Mhe. Dendego, akiwataka waandishi wa habari kusambaza taarifa za tamasha hilo ili ujumbe uwafikie Watanzania na watu duniani kote.
Katika hatua nyingine, Afisa Utalii Mwandamizi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Bi. Irene Mville, amewasilisha mapendekezo ya maeneo ya vivutio vya utalii yaliyobainishwa katika wilaya zote tano za Mkoa wa Singida, ambapo jumla ya vivutio 56 vimeainishwa. Amesema Wizara imependekeza Singida kutambulishwa kwa jina la “The Land of Queen Liti”, likitokana na historia ya kipekee ya Liti Kidanka, huku akieleza kuwa bado kuna vivutio vingine vinavyohitaji utafiti na nyaraka za ziada ili kuweka kumbukumbu zake vizuri.
Bi. Mville ameshauri kuanzishwa kwa kamati za utalii kuanzia ngazi ya kata, wilaya hadi mkoa, zitakazosaidia kubainisha na kufafanua utalii, kuratibu taarifa za vivutio na kuweka mikakati ya kuanza kuvitumia katika shughuli za utalii. Ameeleza kuwa baadhi ya vivutio vilivyobainishwa vinaweza kuanza kutangazwa na kutumika baada ya maboresho ya awali na maandalizi ya taarifa zake.
Wenyeviti wasaidizi wa halmashauri za mkoa huo, wakiwa kama wawakilishi wa wananchi, wameunga mkono kwa asilimia 100 mapendekezo ya Wizara pamoja na kuanzishwa kwa tamasha hilo, wakieleza kuwa ni fursa ya kuifanya Singida kuwa kitovu cha utalii nchini na kuongeza mapato kupitia sekta hiyo. Wajumbe wengine waliohudhuria kikao hicho pia wamepitisha mapendekezo hayo na kuahidi kushirikiana katika utekelezaji wake.
Kupitia tamasha hilo, wananchi wanatarajiwa kunufaika na fursa za ajira na biashara, masoko ya bidhaa na huduma, uwekezaji katika vivutio vya utalii na ongezeko la shughuli za kiuchumi, huku wageni wakipata nafasi ya kutambua historia, utamaduni na vivutio vya Singida. Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, wawakilishi wa Wakurugenzi wa Halmashauri, wakuu wa vitengo na sehemu za Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, maafisa utamaduni na michezo pamoja na wenyeviti wa halmashauri za wilaya.



















No comments:
Post a Comment