Na Glory Kimaro
Katika kuhakikisha wananchi wanashiriki moja kwa moja katika maendeleo ya kiuchumi na kunufaika na rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya maendeleo ya maeneo yao, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Singida imetenga Shilingi milioni 887.4 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya Mpango wa Matengenezo ya Kawaida ya Barabara kwa Kutumia Vikundi vya Kijamii (CBRM), unaolenga kuimarisha miundombinu ya barabara na kuongeza fursa za ajira na kipato kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa kikao cha mpango huo kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, amesema mpango huo ni hatua ya utekelezaji wa vitendo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi endelevu na jumuishi unaogusa makundi mbalimbali katika jamii, hususan vijana na wanawake.
Mhe. Dendego amesema awali kazi za matengenezo ya kawaida ya barabara zilikuwa zikifanywa na wakandarasi wakubwa, hali iliyosababisha sehemu ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya kazi hizo kutonufaisha moja kwa moja wananchi wa Singida. Ameeleza kuwa kupitia CBRM, fedha hizo zitazunguka ndani ya mkoa, kuongeza kipato cha vikundi na kuchochea shughuli nyingine za kiuchumi katika jamii.
Aidha, amevitaka vikundi 41 vilivyosajiliwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na weledi, kutunza vitendea kazi vilivyokabidhiwa na kutumia fursa hiyo kukuza uwezo wao hadi kuanzisha kampuni kubwa zitakazoweza kushindana na kupata kazi hata nje ya mkoa. Amesisitiza kuwa ushiriki wa wananchi katika matengenezo ya barabara utasaidia pia kuzuia uharibifu mkubwa unaoweza kuongeza gharama za Serikali.
“Tunaposema uchumi, unawagusa watu, na ili uwe endelevu na jumuishi, lazima uguse yale makundi maalumu katika jamii. Kupitia programu hii ya TARURA, tumeanza kuitekeleza Dira ya Taifa 2050 kwa vitendo. Haya ni mabadiliko makubwa ya kiuchumi,” amesema Mhe. Dendego.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida, Mhandisi Claver Mwinuka, amesema fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo katika Halmashauri za Iramba, Mkalama, Manispaa ya Singida na Halmashauri ya Wilaya ya Singida. Ameeleza kuwa vikundi 41 vimesajiliwa, ambapo 10 vinatoka Manispaa ya Singida, 10 Halmashauri ya Wilaya ya Singida, 15 Iramba na sita Mkalama. Kila kikundi kitatunza barabara yenye urefu wa takribani kilomita tatu hadi 10, kulingana na hali na mahitaji ya eneo husika.
Mhandisi Mwinuka ameongeza kuwa shughuli zitakazofanywa na vikundi hivyo ni pamoja na kufyeka nyasi, kusafisha mitaro, kuondoa vichaka na uchafu, kurekebisha mabega ya barabara na kufanya matengenezo mengine ya kawaida kwa maelekezo ya TARURA. Amebainisha kuwa mpango huo utasaidia kupunguza uharibifu wa barabara, kuimarisha usalama wa watumiaji na kuhakikisha barabara zinapitika kwa muda mrefu zaidi, huku vikundi vikipewa vitendea kazi vya msingi ili kuimarisha usalama wao kazini.
Nao wawakilishi wa vikundi nufaika hivyo wameahidi kutekeleza majukumu yao kwa bidii na weledi ili kuboresha barabara walizopangiwa na kuongeza kipato cha wanachama wao. Aidha, wamesema fursa hiyo itawawezesha kujikwamua kiuchumi, kutengeneza ajira kwa wengine na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya maeneo yao.
Kikao hicho kilihusu mradi mpya wa matengenezo ya kawaida ya barabara kupitia TARURA, unaohusisha vikundi 41 vinavyoundwa na wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalumu. Mradi huo ulilenga kusainiwa kwa mikataba kati ya TARURA na vikundi husika pamoja na kukabidhiwa vitendea kazi kwa ajili ya kufanya usafi wa barabara na matengenezo madogomadogo ili kuhakikisha barabara zinakuwa salama na zinapitika.

Kupitia mpango huo, wananchi wa Singida wanatarajiwa kunufaika na barabara zinazopitika na kuwa salama mwaka mzima, kupungua kwa gharama na usumbufu wa usafiri, kuimarika kwa shughuli za kiuchumi na kuongezeka kwa ajira na kipato kwa vijana na wanawake. Kikao hicho kimehusisha pia kusainiwa kwa mikataba kati ya TARURA na vikundi husika pamoja na maonesho ya vitendea kazi vilivyotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo. Pia kimehusisha viongozi wa mkoa na wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, viongozi wa taasisi na wawakilishi wa vikundi. Kwa Ujumla kikao kimejadili umuhimu wa ushirikiano katika kuhakikisha barabara zinatunzwa ipasavyo.
Mpango huo unatarajiwa kuimarisha usalama na upatikanaji wa barabara, kuongeza fursa za kiuchumi na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
No comments:
Post a Comment