Mkoa wa Singida umejiandaa kikamilifu kuwa wenyeji wa Maonesho ya saba (7) ya kitaifa ya mifuko ya programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi, yatakayofanyika kuanzia Septemba 8 hadi 14, 2024, katika viwanja vya Bombadia.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego,
amesema kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika ili kuhakikisha wageni kutoka
mikoa mbalimbali wanapokelewa na kuhudumiwa vizuri huku akisisitiza umuhimu wa
wananchi wa Singida kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu.
"Kushiriki katika maonesho haya
ni fursa adimu kwa wananchi wetu wa Singida ...tujiandae kupokea wageni wengi
na hii kwetu sisi ni fursa kubwa kwa wajasiriamali wetu.....," amesema RC
Dendego.
Ameongeza kuwa maonesho haya
yanatoa nafasi ya pekee kwa wananchi kupata uelewa wa kina kuhusu programu
mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi na jinsi wanavyoweza kunufaika nazo
huku akitoa rai kwa wafanyabiashara kutoa huduma nzuri na kuepuka upandishaji wa bei
usioeleweka ili wageni watamani kurudi tena Singida.
Akizungumzia hali ya ulinzi na
usalama amesema, serikali ya mkoa imejipanga kikamilifu ili kuhakikisha usalama wa
wageni na washiriki wote wa maonesho hayo lengo likiwa ni kuboresha nafasi ya
Singida kama kituo cha mikutano na maonesho.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa
Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bi. Beng’i Issa, ameeleza
kuwa maonesho
hayo yatakuwa na taasisi nyingi zinazotoa mikopo na ruzuku kwa ajili ya
uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
"Tuna matarajio makubwa ya watu
kushiriki vizuri na kupata huduma na fursa mbalimbali kupitia programu
mbalimbali na mifuko ya uwezeshaji hapa nchini. Hii itatusaidia kuinua uchumi
wetu binafsi," amesema Bi. Beng’i Issa.
Maonesho hayo yatafunguliwa rasmi na Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, na Uratibu, Mheshimiwa William Lukuvi tarehe 8 Septemba 2024, na kilele chake kitakuwa tarehe 14 Septemba 2024, ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
No comments:
Post a Comment