Tuesday, June 11, 2024

RC SINGIDA AKATAA KUZINDUA BWENI KISA UMALIZIAJI WA UJENZI CHINI YA KIWANGO, AWAAGIZA WATENDAJI KUSIMAMIKA MIRADI KIKAMILIFU.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego, amekataa kuzindua bweni la Wanafunzi wa kike katika shule ya Sekondari Mtekente iliyopo Wilayani Iramba baada ya kubaini kuwa ujenzi huwa wa bweni pamoja na jiko yaliyojengwa na Kampuni inayojishughulisha na ununuzi wa pamba Biosustain mkoani humo kwa zaidi ya shilingi milioni 180 yamejengwa chini ya Kiwango.

Kufuatia hali hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa wa Singida amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Iramba kushirikiana na Kampuni hiyo katika kurekebisha maeneo yote yenye kasoro ikiwemo sakafu ndipo ataenda kuzindua bweni hilo ambalo litakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi wa kike 80 kabla ya shule kufunguliwa.

Amesema ujenzi huo wa bweni limejengwa vizuri lakini umaliziaji ndio mbovu katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye kuta na vyoo hivyo kazi ya maboresho lazima ifanyike haraka kabla ya wanafunzi kurejea mashuleni.

Mheshimiwa Halima Dendego amewasisitiza Viongozi katika ngazi zote Mkoani Singida kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika usimamizi wa miradi kama hiyo hata kama ni ya wafadhili ili kazi iweze kufanyika kwa viwango vinavyotakiwa kulingana na thamani ya fedha.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego (katikati), akikagua na kutoa maelekezo baadhi ya sehemu ya jiko lililojengwa kwaajili ya kuhudumia bweni la shule ya Sekondari Mtekente Wilayani Iramba.

Kuhusu tatizo la Walimu wa shule ya Sekodari Mtekente kutishiwa maisha na baadhi ya wananchi wa kijiji hicho, Mkuu huyo wa mkoa amemwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi wa Wilaya ya Iramba kuchukua hatua haraka za kuwakamata na kuwachukulia hatua wananchi wanaowatishia maisha walimu hao ili kukomesha vitendo hivyo.

Halima Dendego amesema kuwa anataka kuona Wananchi pamoja na Watumishi waliopo mkoani Singida wanafanya kazi na kuishi kwa amani bila kusumbuliwa na mtu yeyote kwa masaa 24 na atakayewasumbua basi lazima awajibishwe kwa kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Nendeni Mkawaambie Vijana wetu huko mtaani nikiona tukio la namna hii linajitokeza tena nitajua la kufanya na msije mkanilaumu, Amesisitiza Halima Dendego.

Mkuu huyo wa mkoa pia amewataka Walimu waendelee kufanya kazi kwa bidii kwa sababu Serikali inajua changamoto wanazokumbana nazo ikiwemo madai yao na Serikali itaendelea kuzitatua changamoto hizo kwa muda muafaka.

Awali Mkuu huyo wa Mkoa ameshiriki kwenye shughuli ya kufanya usafi katika maeneo mbalimbali zoezi lililofanyika katika eneo la soko lililopo mjini Kiomboi wilayani humo lengo likiwa ni kuhamasisha jamii kutunza mazingira ambapo akawaelekeza viongozi wa soko na maeneo mengini kuwajibika ipasavyo katika swala la mazingira ili kuepukana na magonjwa yanayotokana na mazingira machafu.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego, akisalimiana na baadhi ya viongizi pamoja na walimu wa shule ya Sekondari Mtekente mara baada ya kuwasili kwaajili ya uzinduzi wa bweni la shule hiyo Wilayani Iramba.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego, akizungumza kwa msisitizo kuhusu maboresho ya bweni la wasichana lililojengwa katika Sekondari Mtekente Wilayani Iramba.

Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego akiwa kwenye ukaguzi wa ndani ya jiko.

Muonekano wa jiko la kuhudumia wananfunzi wa bweni katika shule ya Sekondari Mtekente wilayani Iramba.



Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego, akizungumza kwa msisitizo kuhusu maboresho ya bweni la wasichana lililojengwa katika Sekondari Mtekente Wilayani Iramba.

Muonekano wa ndani ya bweni hilo.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Singida kukagua na kuzindua bweni.

Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego akizungumza mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa bweni katika shule ya Sekondari Mtekente wilayani Iramba.

Baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mtekente wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida  wakati wa hotuba yake.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego, akiwa mstari wa mbele katika eneo la kuhifadhia taka mjini Kiomboi ili kuhamasisha wananchi utunzaji na maeneo mbalimbali wilayani Iramba na mkoa kwa ujumla kuwa safi ili kuepukana na magonjwa.  

No comments:

Post a Comment