Wednesday, February 28, 2024

RC SERUKAMBA AWATAKA WATENDAJI WA SERIKALI MKOANI SINGIDA KUTIMIZA WAJIBU WAO KWA WAKATI

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba ametoa wito kwa viongozi na watendaji wa Serikali kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kusimamia miradi yote inayotekelezwa katika halmashauri za mkoa huo kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma stahiki.

Wito huo umetolewa leo Februari 28, 2024 wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa Mkoa kilichohusisha Katibu Tawala wa Mkoa huo, Dkt Fatuma Mganga, Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi, Wakuu wa Sehemu na Vitengo kutoka mkoani na wilayani.

Serukamba, amesema haiwezekani fedha zilizoletwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo majengo ya shule, vituo vya afya, barabara halafu kuna baadhi ya watendaji wanachelewesha utekelezaji wake, kwahatua hiyo ameahidi hatomvumilia yeyote atakayehusika kuchelewesha au kukwamisha miradi kukamilika kwa wakati na hatimaye atachukuliwa hatua za kinidhamu.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, akisisitiza jambo wakati wa kikao kazi hicho.

“Nitoe rai kwa viongozi wenzangu, twendeni tukasimamie miradi yote katika halmashauri zetu ili ikamilike kwa muda tuliokubaliana leo hapa, mimi na ‘RAS’ pamoja na timu ya Mkoa tutakuja halmashauri baada ya siku 10 ili kukagua na kuona hatua ilipofikia, ole wake atakayeleta mchezo kwenye jambo hili sitocheka naye". RC Serukamba

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amewahimiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa huo kwenda kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato kutoka katika kila chanzo ikiwemo minada, mazao ya biashara na kuhimiza kutotumia fedha za mapato ya ndani kwa miradi iliyoletewa fedha na Serikali.

Akimalizia hotuba yake Serukamba amewasihi Wakuu wa Wilaya Mkoani humo kwenda kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara katika maduka kuhusu bei za sukari na endapo wakiwabaini wafanyabiashara wanaouza bei ambayo ni kinyume na bei elekezi iliyotolewa na Serikali wawakamate ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Agizo hilo limetokana na operesheni aliyoifanya jana Februari 27, 2024 Wilayani Manyoni ya kuwakamata walanguzi wa sukari ambapo alimkamata mfanyabiashara akiuza mfuko wa sukari wenye kilo 50 kwa bei Sh. 189,000 ambayo ni kubwa ukilinganisha na bei elekezi ya Serikali.

“Tumepata baahati ya kuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan mwenye maono na anayejali wananchi wake kwa mtu mmoja mmoja analetea fedha nyingi za miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani kwetu hivyo hakuna sababu ya kutokamilisha na kutotekeleza wajibu wetu ipasavyo”. RC Serukamba amesema

Kwaupande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga, amewasisitiza watendaji hao wa Serikali hususan Wahandisi wa halmashauri, maafisa mipango pamoja na maafisa manunuzi kuwa wazalenda wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi kwa kutumia fedha kulingana na mahitaji halisi ya fedha sambamba na kuwa na dhamira ya dhati ya ukamilishaji miradi.  

MATUKIO KATIKA PICHA

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, wakati wa kikao kazi hicho.


Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga, akifuatilia jambo katika moja ya taarifa za halmashauri wakati wa kikao kazi hicho.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Asia Messos, akitoa taarifa wakati wa kikao kazi hicho.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, akifuatilia jambo kwenye moja ya taarifa ya halmashauri wakati wa kikao hicho.



Kikao kazi kikiendelea.

No comments:

Post a Comment