Thursday, December 07, 2023

MAAFISA KILIMO WATAKIWA KUWASAJILI WAKULIMA KWENYE DAFTARI LAO

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amewataka Maafisa Ugani kuhakikisha wanaendesha zoezi la kusajili Wakulima katika daftari linaloonesha idadi yao ili kuanisha uhalisia wa majukumu ya shughuli zao za Kilimo na kuwatambua kupitia kwenye maeneo wanayoishi.

Serukamba amesema hayo, alipokutana na Watendaji wa Kata, Vijiji na Wataalamu wa Kilimo wa Halmashauri ya itigi Wilayani Manyoni kwa lengo la kujadili msimu mpya wa Kilimo (2023/24), katika Kikao kilichofanyika Ukumbi wa Halmashauri ya Itigi ili kuongeza uzalishaji wa mazao na maeneo mapya ya kilimo.

Aidha Serukamba, alitumia fursa hiyo kuwataka Maafisa Kilimo wakawahamasishe wakulima kupanda miti kwenye mipaka ya mashamba yao kama njia mojawapo ya kutunza na kuhifadhi mazingira kwenye maeneo yanayowazunguka.

“Suala hili la mazingira naomba sana kila mmoja wetu atekeleze…ni muhimu pia kwa Taasisi za Serikali zikiwemo Shule, Zahanati na Vituo vya Afya kupanda miti pembezoni mwa jengo…” RC Serukamba

Serukamba amewataka Maafisa Kilimo kutoka maofisini kwenda vijijini kuelimisha wakulima umuhimu wa matumizi ya mbolea na mbegu bora ambapo amesisitiza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameleta mbolea yenye ruzuku hivyo wakulima isipowafikia ni kosa ambalo hatoweza kulivumilia kwa atakaye sababisha. 

Naye mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Manyoni alimshukuru Serukamba na kumhakikishia maeneo yaliyoainishwa kwenye kikao hicho idadi ya ekari kisichopungua 4,000, zote zitalimwa na atahakikisha anasimamia wakulima kutumia mbegu bora na mbolea, ili kuongeza uzalishaji mazao shambani.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, akisisitiza jambo kwa Watendaji wa Kata, Vijiji na Wataalamu wa Kilimo wa Halmashauri ya Itigi Wilayani Manyoni kwa lengo la kujadili msimu mpya wa Kilimo (2023/24), katika Kikao kilichofanyika Ukumbi wa Halmashauri ya Itigi ili kuongeza uzalishaji wa mazao na maeneo mapya ya kilimo 7 Disemba 2023.

Watendaji wa Kata, Vijiji na Wataalamu wa Kilimo wa Halmashauri ya Itigi Wilayani Manyoni wakiwa katika kikao kilichofanyika Ukumbi wa Halmashauri ya Itigi kwa lengo la kujadili msimu mpya wa Kilimo (2023/24) ili kuongeza uzalishaji wa mazao na maeneo mapya ya kilimo 7 Disemba 2023.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, leo Disemba 7, 2023 amehitimisha ziara yake ya kuhamasisha Kilimo chenye tija Mkoani humo katika Wilaya ya Manyoni ambapo amekutana na Watendaji wa Kata Vijiji na Maafisa Kilimo pamoja na wataalamu mbalimbali wa Halmashauri ya Itigi na Manyoni.  

No comments:

Post a Comment