Monday, December 11, 2023

JAMII MKOANI SINGIDA, YAHIMIZWA KUCHUKUA HATUA THABITI KUZUIA VITENDO VYA UKATILI.

SERIKALI Mkoani Singida kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imetoa wito kwa kila mwananchi mkoani humo kutumia nafasi aliyonayo katika familia, jamii ama taasisi kuchukua hatua thabiti ili kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo kutoa taarifa haraka na kushirikiana na wahusika pindi wanapoona mtu anafanyiwa ukatili.

Wito huo umetoa katika kilele cha Maadhimisho ya Kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili yaliyofanyika Kimkoa Disemba 10, 2023 katika ukumbi wa mikutano Chuo cha Uhasibu kilichopo katika Manispaa ya Singida, ambapo mgeni rasmi alikuwa Katibu Tawala Mkoa Dkt. Fatuma Mganga aliyewakilishwa na Bw. Steven Pancras, ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na Rasilimali Watu Mkoa.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa, Bw. Pancras amezisisitiza jamii pamoja na taasisi za umma na binafsi kuwa na hatua za makusudi za kuongeza ulinzi kwa wanawake na watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia ambapo amehimiza jamii kutoa taarifa haraka pamoja na kushirikiana na Serikali sambamba na wadau ili vitendo hivyo vikomeshwe.

“Sisi wana Singida lazima tujenge nguvu ya pamoja kwani mkoa unahitaji kuwekeza zaidi katika juhudi mbalimbali ili kukomesha ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto kwa kuwa bado tatizo hili ni kubwa na linaendelea” Amesema Pancras

Akieleza kwa msisitizo amesema, vitendo vya ukatili vinaathiri watu wengi hasa wale walio katika makundi maalumu yanayoonewa kama, Watoto, Wanawake na Watu wenye ulemavu ambapo madhara yake ya vitendo hivyo ni makubwa kama vile athari za kiafya, kiuchumi na kijamii, watoto kuacha shule pamoja na mimba za utotoni hivyo ni iungane kwa pamoja kupinga ukatili.

“Kauli mbiu ya Kampeni hii kwa mwaka 2023 ni Wekeza: Kuzuia Ukatili wa Kijinsia. Wito huu unasisitiza ya kwamba vitendo vya ukatili vinazuilika kwa kutoa ushirikiano kwa wahusika, kinga ni bora kuliko tiba” Amesema Pancras

Akizungumzia utafiti uliyofanyika Tanzania (The 2009 National Survey on Violence against Children) amesema unaonesha kuwa asilimia 28 ya wasichana na 13 ya wavulana wamefanyiwa ukatili wa kingono ambapo ukatili huo hutokea katika mazingira ya nyumbani.

Hata hivyo ameeleza kuwa asilimia 73 ya wasichana na 72 ya wavulana wamefanyiwa ukatili wa kimwili na wengi wao zaidi ya asilimia 60 hufanyiwa na ndugu wa karibu na asilimia 40 ya ukatili hufanyiwa shuleni. Amefafanua kuwa utafiti huo ulionesha  robo (¼) ya watoto wa kitanzania wavulana na wasichana wamefanyiwa ukatili wa kihisia au kisaikolojia.

Utafiti uliyofanyika 2022 (Tanzania Demographic and Health Survey) zinaonesha 40% ya wanawake katika umri wa miaka 15-49 wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili wakati 17% wamefanyiwa ukatili wa kingono na 44% walifanyiwa ukatili wa kimwili au kingono na wenza wao ambapo Mkoa Singida takwimu zinaonesha wanawake wenye umri kati ya 15-49 waliofanyiwa ukatili wa kingono, kimwili au kihisia na wenza wao ni asilimia 45”.

Akimalizia hotuba yake Pancras amesema, Serikali imefanya jitihada mbalimbali za kuzuia ukatili ikiwemo na pamoja na kuwa na mpango wa kitaifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wananwake na watoto (MTAKUWWA II) inayolenga kufikia malengo ya kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa 50% ifikapo 2028.

Hivyo Mkoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na SMAUJATA, Jeshi la Polisi, vyombo vya habari pamoja na wadau wa maendeleo wameelekeza mikakati mbalimbali ya kupinga na kutokomeza ukatili ikiwemo uanzishaji wa kamati za Ulinzi na Usalama za wanawake na watoto ngazi zote za jamii (MTAKUWWA) ili kwa pamoja kupinga ukatili.

Imeelezwa kuwa, katika Siku 16 za kupinga Ukatili kwa mwaka 2023 Mkoa umeweza kutekeleza na kusimamia afua mbalimbali zikiwemo; Elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia imetolewa katika maeneo mbambali kwenye mikutano ya hadhara ma shuleni kwa halmashauri zote saba (7).

Kongamano la Elimu dhidi ya vitendo vya ukatili lilojumuisha watu takribani mia tatu (300) lilifanyika katika halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Mkoa kupitia halmashauri ya Wilaya ya Manyoni umeweza kushiriki katika msafara wa kutoa elimu dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia (Gender Caravan) ambapo vituo vya bodaboda, shuleni na kwenye masoko vilipatiwa elimu hiyo.

Aidha zaidi ya miche mia nane (800) ya miti ilipandwa katika halmashauri ya Wilaya ya Ikungi katika vijiji vya Dung’unyi, Puma na Ikungi.

Kampeni ya Siku 16 za kupinga Ukatili wa kijinsia ni Kampeni kabambe ya Kimataifa inayoongozwa na kituo cha Kimataifa cha Wanawake katika uongozi tangu 1991. Kampeni ilitokana na Mauaji ya kinyanya ya Wanawake wa Mirabelle yaliyofanyika nchini Dominica mwaka 1960. Novemba 1991, umoja wa Mataifa ulitenga siku hiyo kama siku ya kimataifa ya kupinga ukatili dhidi ya Wanawake.

 

No comments:

Post a Comment