Thursday, November 16, 2023

SERUKAMBA AFANYA ZIARA VIJIJI 15 KWA SIKU MOJA WILAYANI IKUNGI

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, leo Novemba 16, 2023 amefanya ziara katika Wilaya ya Ikungi kwa lengo la kukagua na kutembelea miradi ya Maendeleo ikiwa ni muendelezo wa ziara zake kwa kukutana na wananchi kupitia mikutano ya hadhara kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili.

Ziara hiyo yenye umbali wa zaidi ya Kilomita 400 kwenda na kurudi kutokea makao makuu ya Mkoa, mjini Singida ilihusisha baadhi ya vijiji kikiwemo cha Iyumbu, Makungu, Magungumka, Ufana, Mwankalaja, Kaugeli, Mdughuyu, Mlandala, Mpugizi, Mwaru, Maghonda, Mghungira na Ighombwe.

Akiwa katika kijiji cha Iyumbu kilichopo mpakani mwa Mkoa wa Tabora na Singida, Serukamba alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Kata hiyo fedha za ujenzi wa shule mpya ya Sekondari inayogharimu Sh. Milioni 540/=.

Aidha, licha ya kupokea kero mbalimbali katika kijiji na Kata ya Iyumbu, Mkuu huyo wa Mkoa aliitaka idara ya ardhi Wilayani Ikungi kuhakikisha inatatua mgogoro wa mashamba pamoja na kuyapima maeneo hayo ili kuwapatia wakulima hati miliki.

Pia Serukamba alimtaka Afisa Kilimo wa Wilaya hiyo, Gulisha Msemo, kusimamia zoezi la upatikanaji wa mbolea ya ruzuku hadi kufikia Novemba 20, mwaka huu iwe imewafikia wakulima wote wanaohitaji.

Akiwa kijiji cha Makungu, Kata ya Iyumbu licha ya kuitaka Halmashauri ya Wilaya hiyo kutenga Sh. Milioni Tatu (3,000,000/=) za ujenzi wa miundombinu ya kuvuna maji ya mvua kwa matumizi ya wanafunzi kupata huduma ya choo. Hata hivyo aliitaka RUWASA kumaliza kero ya maji katika kijiji hicho kwa kuchimba kisima kwa ushiriakiano wa Bonde la Kati na Halmashauri ya Wilaya.

Pamoja na kero ya maji kuonekana kuwa changamoto katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa aliiagiza RUWASA, kusimamia zoezi hilo ili kuwaondolea Wananchi adha ya maji, huku pia akihimiza upatikanaji wa mbolea kwa matumizi ya msimu mpya wa kilimo mwaka huu (2023/2024).

Kuhusu mradi wa REA unaoendelea kwenye maeneo mbalimbali Wilayani Ikungi, Serukamba alimwagiza Wakala wa Nishati Vijijini, kusimamia Wakandarasi ili ifikapo Desemba 31, mwaka huu Vijiji vyote vya Wilaya hiyo viwe vimefikiwa na nishati hiyo.

Katika ziara hiyo, Serukamba alifanikiwa kufika kwenye kambi ya wavuvi iliyopo katika kijiji cha Ufana Kata ya Mghungira, walioathiriwa na tukio la baadhi yao nyumba zao kuteketea kwa moto uliyosababisha mtu mmoja kupoteza uhai, na baada ya kuwapa faraja aliwataka kuchukua tahadhari dhidi ya majanga hayo ili kulinda mali na maisha yao.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa, aliwapongeza Wananchi wa kijiji cha Magungumka kwa kutumia nguvu na rasilimali zao kujenga na kupaua jengo la kituo kidogo cha Polisi ambapo alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, kuunga mkono juhudi hizo kwa kuhakikisha kituo hicho kinakamilika na kuanza kutoa huduma haraka.

Kuhusu ujenzi wa miradi ya afya na elimu, Serukamba alipongeza juhudi za Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, kwa kusimamia vyema ujenzi wa Zahanati mbalimbali zilizokamilika na kuanza kutoa huduma na akamuagiza Mkurugenzi kupeleka Wataalamu wa huduma za afya ili Wananchi waanze kunufaika na matunda ya Serikali yao.

Akizungumzia Sekta ya Elimu, Mkuu wa Mkoa huyo aliitaka Halmashauri ya Wilaya hiyo kuunga mkono juhudi za Wananchi pale ambapo wameweza kuanzisha ujenzi wa vyumba vya madarasa kupitia shule shikizi ili baadaye ziweze kupandishwa hadhi kwa kusajiliwa kuwa shule kamili.

Aidha katika ziara hiyo Wananchi wamemshukuru Mkuu huyo wa Mkoa kwa kufanya uwamuzi wake wa kwenda kila kijiji ambapo amekuwa na utaratibu wa kukutana na Wananchi moja kwa moja kwa kuwafuata vijijini ili kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu. 

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA
No comments:

Post a Comment