Tuesday, November 28, 2023

SERUKAMBA AAGIZA KUKAMILIKA KWA VYUMBA VYA MADARASA ILI YATUMIKE KWA WANAFUNZI IFIKAPO JANUARI 2024

 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, amezitaka Halmashauri za Wilaya Mkoani Singida kukamilisha miradi ya maendeleo kwa wakati ikiwemo ya elimu ili wanafunzi wenye sifa ya elimu ya awali na msingi wapate nafasi na watakaofaulu waendelee na elimu ya Sekondari ifikapo Januari 2024.

Serukamba amesema hayo leo Novemba 28, 2023 alipoongea na Wazazi Walezi na Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi katika shule ya msingi Kintandaa muda mfupi baada ya kukagua miradi ya maendeleo kwenye kijiji cha Irisya, Msimii, Kipunda na Kintandaa ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika kila kijiji Mkoani humo.

Mkuu huyo wa Mkoa alilazimika kutoa maelekezo hayo baada ya kujionea ujenzi wa vyumba vya madarasa ya shule ya msingi Kintandaa na ambayo yapo kwenye hatua mbalimbali za ujenzi wakati umebakia mwezi mmoja pekee wanafunzi waanze muhula mpya wa masomo kote nchini.

“Mkurugenzi, lijulishe baraza lako la Madiwani juu ya ujenzi wa vyumba vya madarasa…hakikisha mnakamilisha mapema kabla ya Disemba 31 mwaka huu, ili ifikapo mwezi wa kwanza mwakani, wanafunzi waweze kuyatumia katika masomo yao,”alisema Serukamba.

Aidha katika kituo cha afya Irisya, Serukamba, alimtaka Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Alli Mwanga, kulielekeza Baraza la Madiwani liidhinishe fedha za kukamilisha miradi ya Zahanati na vituo vya afya ili wananchi waanze kunufaika na matunda ya Serikali yao ya awamu ya sita.

“Kwenye miradi hii yote, hakikisheni mnaisimamia vizuri na kuifuatilia mwanzo hadi mwisho, ili iweze kuendana na kasi, ubora, thamani ya fedha na kiwango kinachostahili, kwa lengo la kuleta tija kwa jamii yetu tunayoitumikia,” alisisitiza Serukamba.

Mapema katika mkutano huo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Alli Mwanga, aliipogeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwaletea wananchi maendeleo kupitia miradi ya afya elimu maji na miundombinu ya barabara.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, sisi wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, pamoja na mambo mengi ya maendeleo yanayoendelea hivi sasa, tunamshuru sana Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutupatia fedha za kutosha kwa ajili ya miradi mbalimbali inayotekelezwa” alisema.

Mwenyekiti huyo, alitumia muda huo pia kuwaomba wananchi waendelee kumuunga mkono Rais, kutokana na kazi kubwa ya maendeleo anayoifanya lengo likiwa ni kwa ajili ya kuwajali Watanzania, na bila kuwabagua kwa misingi ya dini na kabila lake la asili.

Ziara hiyo ni mahususi kwa Mkuu huyo wa Mkoa, kutembelea vijiji vyote 441 vya Mkoa wa Singida, huku katika awamu ya kwanza akiwa amekamilisha kukutana na wananchi wa vijiji zaidi ya 61, kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazoikabili jamii.


Moja ya mwananchi wa Kijiji cha Kipunda akiuliza swali wakati wa ziara hiyo.






Mkuu wa Wilaya ya Ikingu Thomas Apson akizungumza wakati wa ziara hiyo.

Ziara ikiendelea.

No comments:

Post a Comment