Wednesday, November 29, 2023

BASI LA KAMPUNI YA ALLY'S STAR LAGONGA INJINI YA TRENI NA KUUA ABIRIA 13 WILAYANI MANYONI SINGIDA

Watu 13 wamefariki Dunia katika ajali iliyohusisha basi la kampuni ya Ally’s Star kugonga Injini ya Treni katika makutano ya barabara kuu ya Manyoni - Singida, kwenye eneo la Manyoni mjini, mkoani Singida, leo Jumatano Novemba 29, 2023.

Baada ya ajali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, akiongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa alifika kwenye eneo la tukio ambako alishuhudia na kupata nafasi ya kuzungumzia tukio hilo.

Akiwa kwenye eneo la tukio Serukamba, alieleza kusikitishwa na ajali hiyo alipofika kwa ajili ya kuwatembelea na kuwapa pole kwa ndugu wa marehemu na majeruhi waliolazwa hospitali ya Wilaya ya Manyoni na waliopata rufaa kwenda hospiatli ya St. Gaspar Itigi na kuwaombea wapate nafuu majeruhi waweze kuendelea na shughuli za kujenga taifa..

Hata hivyo Serukamba, ametoa rai kwa watumiaji wa vyombo vya moto hususani madereva wa mabasi kuzingatia sheria alama na taratibu za barabarani hasa kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka.

Aidha Serukamba alitumia fursa hiyo kuwashukuru Wauguzi na Madaktari wa hospitali ya Wilaya ya Manyoni na Itigi, kwa kujitoa kwa kila hali katika kuwahudumia majeruhi walionusurika kwenye ajali hiyo.

Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa, alisema tukio hilo limetokea majira ya saa 10 alfajiri, wakati basi hilo lenye namba za usajili T 178 DVB likijaribu kukatiza njia ya reli eneo la Manyoni mjini kisha kugongana na Injini ya Treni.

Alisema kuwa basi hilo likiwa katikati ya njia ya reli ghafla liligongwa na Injini ya Treni kilichokuwa kikirudi Manyoni mjini kutokea kituo cha Aghondi na hivyo kusababisha vifo na majeruhi waliokuwemo kwenye basi la Ally’s.

Kamanda Mutabihirwa amesema kuwa basi hilo lilikuwa na jumla ya abiria 57 na waliopoteza maisha ni abiria 13 (wanawake 6, wanaume 7) huku majeruhi wakiwa 32 na wengine waliobakia walinusurika na kuendelea na safari.   


















No comments:

Post a Comment