Walimu wa shule za Serikali Mkoani Singida watakiwa kuhakikisha wanafuta daraja la sifuri na daraja la nne kwa kufanya kazi kwa bidii, kuwashirikisha wazazi na wanafunzi wenyewe.
Akiongea katika kikao kazi kilichowakutanisha Walimu wa
shule za msingi, sekondari na wadhibiti ubora uliofanyika leo katika ukumbi wa
mikutano wa RC Mission uliopo mjini Singida.
RC Serukamba amesema uondoaji wa madaraja hayo ya elimu
utawezekana kwa kuacha uzembe, kuwahi kazini na kuwa na tabia ya kupata
mrejesho baada ya kufundisha huku akiwataka wazazi kuhakikisha wanafunzi
wanapata chakula mashuleni.
Hata hivyo amewataka Maafisa elimu wa kata kuhakikisha
wanatembelea mashule na kuhakikisha kila mwalimu anatimiza majukumu yake huku
akiwakumbusha wadhibiti ubora kutowadhibiti walimu pekee badala yake waangalie
changamoto zinazo wakabili walimu.
Aidha amewakumbusha walimu kahakikisha kwamba katika Mkoa wa
Singida hakutakuwa na Mwanafunzi atakayemaliza
darasa la Saba bila kujua kusoma na kuandika.
Katika kuboresha Elimu RC Serukamba ameeleza nia yake ya
kutaka kuanzisha mashindano kwa Shule za Sekondari ambapo shule ambayo
haitapata daraja sifuri na daraja la nne watapata zawadi itakayo gawanywa kwa
walimu wote wa shule husika.
"Umefika wakati sasa wadhibiti ubora kuhakikisha
tunapata elimu bora kwa kuwa Serikali imeshawekeza vya kutosha katika majengo
na miundombinu ya shule, umefika wakati Serikali kuwekeza katika ujuzi ili
kuleta ubobezi katika masomo yanayofundisha" alieleza RC Serukamba.
Hata hivyo amewataka walimu kuendeleza juhudi na utamaduni
wa kusoma vitabu badala ya kutumia mitandao ya kijamii.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida Mwl. Dorothy Mwaluko amesema Mkoa una jumla ya Walimu 7492 ambapo wa shule ya msingi ni 5166 na Sekondari ni Walimu 2326.
Amesema uwepo wa walimu hao kumesababisha kuanza kuboresha elimu
ambapo amesema kwa kidato cha sita
ambapo ufaulu umefikia daraja la kwanza na kwa wanafunzi wa darasa la nne
ameeleza kwamba waliofanya mtihani ni asilimia 93 na waliofaulu ni asilimia 82.
Hata hivyo RAS amesema katika zoezi la kuboresha elimu mkoani
hapo tayari wameanzisha mkakati maalum ambapo utaboresha mahudhurio ya Walimu
na Wanafunzi, ujenzi wa miundombinu na kuboresha uwajibikaji.
Aidha Mwaluko amesema tayari wameshaanza mafunzo ya Walimu
ambapo jumla ya Walimu 1972 kati ya 7000 wameaanza kupata mafunzo ya kuwajengea
uwezo.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Awali na Msingi TAMISEMI
Suzan Nusu ameagiza kuendelea kutolewa kwa Mafunzo endelevu ya walimu kazini
(Mewaka) ndani ya shule ili kujengeana uwezo na kuboresha Elimu na ufundishaji.
Mkutano huo ulihudhuriwa na jumla ya walimu 1956 kutoka Wilaya
zote za Mkoa wa Singida na kuhusisha walimu wa shule ya msingi, sekondari, Tume
ya Utumishi wa walimu na wadhibiti ubora.
No comments:
Post a Comment