Saturday, November 26, 2022

Kituo cha Afya Ntuntu Wilayani Ikungi kuanza kutoa huduma

Wananchi wa kata ya Ntuntu Wilayani Ikungi wanatarajia kuanza kupata huduma za kitabibu katika Kituo kipya cha Afya cha Ntuntu baada ya Ujenzi wake kukamilika kwa asilimia 99.

Akiongea hivi karibuni wakati wa ziara yake Mkurugenzi wa huduma za Afya Lishe na ustawi wa jamii kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR- TAMISEMI) Dkt. Ntuli Kapolongwe  amesema ifikapo Jumatatu ya tarehe 28 Novemba kituo hicho kiwe kimeanza kazi za kuhudumia wananchi.

Aidha ameeleza kwamba hatua ya Kituo hicho iliyofikiwa inastahili kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo hayo wakati vitu vidogo vidogo vilivyobaki vikiendelea kukamilishwa.

Hata Hivyo Dkt. Kapolongwe ameagiza Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa kushirikiana na Mganga Mkuu wa Mkoa kuendelea na maandalizi ya kupokea vifaa tiba ili ifikapoa November 28, 2022 huduma ziwe zimeanza na wananchi wanapata matibabu.

"Tumeambiwa jengo limefikia asilimia 99 kukamilika kwa hatua hii ni lazima huduma zianze  kutolewa hata kama kuna vitu vichache vya kumalizia" alisema

Hata hivyo ameendelea kueleza kwamba Serikali ipo hatua ya mwisho ya kuleta vifaa tiba katika Kituo hicho ambapo amesema kufikia Jumatatu vitakuwa vimeshafika hapo.

"Serikali ipo kwenye hatua za mwisho za uletaji wa vifaa tiba mbalimbali katika kituo cha afya hivyo wananchi waanze kupata huduma"  alisema Dkt.  Kapologwe.

Dkt. Kapologwe  ameipongeza  Halmashauri ya Ikungi na timu nzima ya usimamizi wa ujenzi wa Kituo hicho cha Afya kwa ukamilishaji mzuri wa majengo 3 ya awamu ya kwanza (Jengo la Wagonjwa wa Nje OPD, Jengo la Maabara na kichomea taka) ambao mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 99% .

Aidha  majengo  matatu mengine ni pamoja na  jengo la Wodi ya Wazazi (Maternity), jengo la upasuaji (Theatre) na jengo la kufulia (Laundry)  ambapo ujenzi huo umefikia zaidi ya asilimia 60%  huku Dkt. Kapolongwe akiwataka kuongeza kasi ya ujenzi ili kufikia Disemba 30 majengo hayo yawe yamekamilika.

Ujenzi wa Vituo vya afya ni moja ya mkakati na kipaumbele cha Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya katika maeneo ya karibu na makazi yako.



No comments:

Post a Comment