Saturday, August 13, 2022

TARURA Mkoa Singida wamepongezwa kwa jitihada wanazozifanya kufungua barabara mpya na kuboresha zilizochoka

 

Wakala wa barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoani Singida wamepongezwa kwa jitihada wanazozifanya kufungua barabara mpya na kuboresha zilizochoka  huku wakijenga vivuko mbalimbali ili kurahisisha maisha kwa wananchi Mkoani hapo.

Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 13.08. 2022 na Makamu Kiongozi Mbio za Mwenge wa Uhuru Emanueli Ndege Chacha wakati wa ukaguzi na uzinduzi wa daraja na Barabara ya  Utaho Makiungu katika Kijiji cha Mnyinga Wilayani Ikungi.

Akihutubia wananchi walihudhuria kupokea Mwenge wa Uhuru Ndege Chacha amesema pamoja na changamoto kidogo zilizojitokeza katika Ujenzi wa daraja hilo amewapongeza TARURA kwa kujitoa na kufanya kazi kwa umakinifu mkubwa.

Katika ukaguzi wa daraja hilo Mwenge wa Uhuru umebaini changamoto kadhaa zikiwemo kukosekana kwa ukingo wa daraja ambapo ameagiza kujengwa haraka ili daraja liweze kudumu kwa muda mrefu.

Hata hivyo Kiongozi wa Mbio za Mwenge ameagiza Barabara hiyo kuboreshwa ikiwemo baadhi ya maeneo ambayo yameonekana kuwa mabonde ifikapo mwisho wa mwezi Agosti 2022.

Kwa upande wake Mhandisi wa Wilaya ya Ikungi Ally Mimbi amesema daraja hilo limejengwa kwa nondo na zege na kugharimu kiasi cha Tsh.Milioni 112.1 zitokanazo na tozo.

Aidha Mhandisi Mimbi amesema kwamba daraja hilo litawasaidia wananchi wa kijiji cha Kituntu Siuyu, Makiungu na Makotea katika kufanya shughuli za kiuchumi na Biashara.

 

Mwisho

No comments:

Post a Comment