Tuesday, August 16, 2022

SERIKALI Mkoa wa Singida imetenga Sh.Milioni 342.8 kwa ajili ya kutengeneza shughuli za lishe ambapo ni sawa na Sh. 1,239 kwa kila mtoto wa chini ya miaka mitano

SERIKALI Mkoa wa Singida imetenga Sh.Milioni 342.8 kwa ajili ya kutengeneza shughuli za lishe ambapo ni sawa na Sh. 1,239 kwa kila mtoto wa chini ya miaka mitano ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na tatizo la  utapiamlo na udumavu kwa watoto wadogo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, alisema hayo wakati wa makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2022  kati ya Mkoa wa Singida na Mkoa wa Dodoma yaliyofanyika katika shule ya msingi Bahi Wilayani Bahi mkoani Dodoma.

Alisema tatizo la utapiamlo limepungua kutoka asilimia 39 mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 29 lakini bado wataalamu wanaendela kutoa elimu huku wengine wakiendelea kuchunguza sababu za ziada za uwepo wa changamoto hiyo.

Serukamba alisema kwamba jumla ya wakina mama au walezi 422,275 sawa na asilimia 93.4 kati ya 452,061 wamepewa elimu juu ya unyonyeshaji wa watoto wachanga na wadogo.

"Serikali kupitia Mkoa wa Singida bado watafiti wanadelea kuchunguza sababu zinazochangia uwepo wa changamoto ya utapiamlo na udumavu kwa watoto wadogo huku ikiendela kutoa elimu katika ngazi tofauti lengo likiwa ni kuondoa tatizo hilo," alisema.

Serukamba alisema tarifa za kitaifa za demografia zinazofanyika kila baada ya miaka mitano zinaonesha changamoto kubwa ni ukondefu ambapo ni asilimia 4.2 na uzito kuwa pungufu kwa asilimia 18.2.

Alisema mkoa unaendelea kudadisi visababishi vya tatizo hilo la lishe duni katika jamii kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa lishe ili kufanya tafiti za kina kuondokana na tatizo hilo.

Mkuu huyo wa mkoa ameziagiza Halmashauri zote za mkoa huu kuendelea kufanya usimamizi shirikishi kwa wazazi na walezi ili kuongeza uelewa ambao utasaidia kupunguza au kuondoa changamoto hiyo.

Alisema mkoa umejipanga kuendelea kutoa elimu kupitia majukwaa mbalimbali yakiwemo vyombo vya habari kuhusiana na elimu ya lishe kwa wajawazito na akina mama wanaonyonyesha na vijana balehe.

Serukamba amezitaka halmashauri zote za Mkoa wa Singida kuendelea kufanya kaguzi za chakula ikiwa ni pamoja na chumvi zenye madini ya joto.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment