Thursday, August 04, 2022

RC Singida akabidhiwa ofisi rasmi, atoa maagizo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri mkoani humo

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba  leo ameziagiza Halmashauri zote za Mkoa huo kuhakikisha kwamba kila Mwananchi Mkoani hapo anakuwa na kadi ya afya kama hatua mojawapo ya kuboresha za Wananchi hao.

Agizo hilo amelitoa leo wakati wa makabidhiano ya ofisi baina yake na  aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Binilith Mahenge hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi hiyo.

Amesema Serikali imetoa fedha nyingi kujenga vituo vya Afya Zahanati na Hospitali lengo likiwa ni kutoa huduma za Afya kwa wananchi hivyo ni muhimu kuhakikisha wananchi wanapata Bima za Afya ili waweze kupata huduma hizo kwa urahisi.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba   akizungumza na Watumishi wa Umma mkoani Singida mara baada ya kukabidhiwa ofisi rasmi katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

'"Moja ya mambo ambayo nitaanza nayo katika kazi yangu ya Mkuu wa Mkoa ni kuhakikisha kila mwananchi anapata Bima ya Afya, ambapo gharama yake ni sawa na kuku watatu"

Alisema Serukamba swala la Afya ni mtaji mkubwa sana kwa wananchi katika kuleta maendeleo hivyo ni jukumu la kila kiongozi kuhamasisha    wananchi kupata kadi ya afya.

Sambamba na hilo RC Serukamba ameagiza Halmashauri hizo kuongeza vyanzo vya  ukusanyaji wa mapato na kuacha kukadiria  viwango vidogo vya makusanyo huku akiongea kuacha kuangalia asilimia na badala yake waangalie wingi wa fedha.

Amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri hizo kuhakikisha mapato yanaongezeka kwa kuwa vyanzo vipo ila havijatiliwa mkazo.

Aidha RC Serukamba amezitaka Taasisi zinazohusika na Barabara zikiwemo Tanroads na TARURA kwa kushirikiana na Halmashauri kuhakikisha mji unakuwa safi hasa katika Barabara zetu na kuzuia utupaji wa taka kiholela.

Amesema katika kipindi cha wiki moja anataka Mazingira  yawe safi katika Barabara zote za lami pamoja na sehemu za mjini.

Kwa upande wake Dkt Binilith Mahenge aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo aliwashukuru Watumishi na wananchi wote kwa ushirikiano waliompa wakati wa uongozi wake na kuwasihi kutoa ushirikiano mkubwa kwa Mkuu wa Mkoa wa sasa.

Katika taarifa yake Dkt. Mahenge amemueleza Mkuu wa Mkoa kwamba shughuli kubwa inayokaribi Mkoani hapo ni msimu wa kilimo ambapo ameeleza kwamba wananchi wanajiandaa kwa msimu wa kilimo na mpango ulikuwa ni kugawa mbolea za ruzuku baada ya kuwasajili wakulima.

Amesema Singida ina wananchi na watumishi ambao ni  wachapakazi na wanaopenda maendeleo hivyo anaamini mafanikio makubwa yanaweza kupatikana.

Baada ya makabidhiano hayo RC Serukamba alitembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Hospitali ya wilaya ya Ikungi, Veta, ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Singida na Hospitali ya Mkoa Mandewa.

MATUKIO KATIKA PICHA

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge akizungumza na watumishi wakati wa makabidhiano.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akizungumza na watumishi wakati wa makabidhiano.


Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko akizungumza wakati wa hafla ya mapokezi na makabidhiano ya ofisi baina ya Mkuu wa Mkoa  Peter Serukamba na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Dkt. Binilith Mahenge iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano mkoani hapo.






Picha za pamoja


Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (wa pili kutoka kushoto) wakati wa ziara yake ya kukagua Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida iliyopo Mandewa Mjini Singida mara baada ya kukabidhiwa ofisi Agosti 04, 2022 



Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (Kushoto) wakati wa ziara yake ya kukagua Hospitali ya Wilaya ya Ikungi 



No comments:

Post a Comment