Tuesday, July 26, 2022

RC MAHENGE AFUNGA MAFUNZO YA WAKUFUNZI WA SENSA YA WATU NA MAKAZI MKOA S...


Wakufunzi wa Sensa Mkoani Singida waliohitimu mafunzo ya ukarani wametakiwa kuwa wavumilivu katika utekelezaji wa zoezi hilo ili kupata taarifa na takwimu sahihi ambazo zitasaidia Serikali kupanga matumizi sahihi ya wananchi wa Mkoa huo.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dr. Binilith Mahenge katika ukumbi wa mikutano wa VETA wakati akifunga mafunzo ya wakufunzi wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 yaliyodumu kwa siku 21 mfululizo.

RC Mahenge amebainisha kwamba zitajitokeza changamoto ndogo ndogo wakati wa utekelezaji wa zoezi la Sensa ikiwemo mtu kutokuwa na haraka ya kujieleza au ucheleweshaji wa muda Karani asije akaweka data za uongo ili kuokoa muda kwa sababu itakuwa ni hasara kwa Taifa.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dr. Binilith Mahenge akiwahutubia Wakufunzi wa Sensa wa Mkoa Singida waliohitimu mafunzo ya ukarani.

Amesema isije ikatokea kwa namna yeyote Karani akatengeneza taarifa ili mradi awahi kwenda kwenye kaya nyingine hivyo akawataka Makarani hao kuwa na uvumilivu mkubwa ili kazi ikamilike kwa usahihi.

"Hatutahitaji data za kupika Serikali imejitoa kuhakikisha mnapata mafunzo na mmepatiwa vitendea kazi "vishkwambi." Alisema

Hata hivyo RC Mahenge aliwapongeza wakaguzi hao kwa ufaulu huku akiwaabia watumie bahati waliyoipata kuisaidia Serikali kufikia malengo yake.

DC wa Singida Mhandisi Paskasi Muragili akizungumza na Wakufunzi wa Sensa wa Mkoa Singida waliohitimu mafunzo ya ukarani.

Kwa upande wake DC wa Singida Mhandisi Paskasi Muragili alisema kwamba kwa mafunzo yaliyotolewa hawategemei jambo lolote kuharibika kwa kuwa pamoja na masomo ya darasani lakini wakufunzi hao walipata kujifunza kwa vitendo katika Kijiji cha Msisi.

Amewataka wakufunzi hao kwenda kuwafundisha wengine katika ngazi ya Wilaya kama ilivyofanyika kwao ili kuhakikisha hawapotezi maana halisi iliyopangwa.

Mratibu wa Sensa Mkoa wa Singida Naing'oya Kipuyo akitoa taarifa ya mafunzo hayo.

Awali akitoa taarifa ya mafunzo hayo Mratibu wa Sensa Mkoa wa Singida Naing'oya Kipuyo alisema wahitimu hao wamefaulu kwa asilimia 70 ambapo walipata elimu juu ya matumizi ya madodoso manne yakiwemo  dodoso la makundi maalum, ambalo linahusu ukusanyaji wa taarifa za makundi ambayo hayawezi kuhesabiwa na madodoso ya kawaida.

Kipuyo amesema wakufunzi hao wapatao 215 wanatarajia kwenda kuwafundisha Makarani ambao ndio watakuotumika katika zoezi la kuhesabu watu na makazi.

Kwa upande wake Neema Luphebia Mkurugenzi wa Sensa Mkoa wa Singida ameiomba jamii kuhakikisha wanajitokeza kuhesabiwa kwa kuwa ni zoezi ambalo halichukui muda mrefu na lina usiri mkubwa ndani yake.

Naye Ramadhani Mridho Katibu Mkuu wa shirikisho la Walemavu Mkoa wa Singida amawaomba wazazi kutowaficha watoto wenye ulemavu ili waweze kuhesabiwa Serikali iweze kutenga bajeti zao.

Wakufunzi wa Sensa Mkoa wa Singida waliohitimu mafunzo ya ukarani 2022 wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo (hayupo pichani) wakatika akihutubia.


Mwisho.

No comments:

Post a Comment