Saturday, July 16, 2022

Katatueni kero za wananchi vijijini – Waziri Mkuu

 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassimu Majaliwa Majaliwa akizungumza na wananchi katika Kituo cha Afya Mtoa mara baada ya kuweka jiwe la Msingi mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Mtoa wilayani Iramba.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassimu Majaliwa Majaliwa amewataka wafanyakazi wa Halmashauri ya Iramba kuwafuata wananchi vijijini ili kuwasikiliza na kutatua kero zao badala ya kuwasubiri wananchi maofisini.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo akiwa katika muendelezo wa ziara yake katika Kata ya  Mtoa Wilayani hapo wakati wa  kuweka jiwe la msingi katika kituo cha Afya cha Mtoa  kilicho gharimu Tsh. Milioni 662

Amesema  kwa jographia ya Wilaya ya Iramba  vijiji vipo mbali na ofisi za Serikali jambo ambalo inawagharimu fedha nyingi kufika kwenye ofisi hizo kupata huduma.

"Leo mimi nimetoka ofsini kwangu nimekuja Kata ya Mtoa kutatua kero za Wananchi sasa na nyie watumishi wa umma mtoke ofsini mkawahudumie wananchi huko walipo" Alisema

Aidha amewataka watumishi kuwa waaminifu na kusimamia maadili ya utumishi wa umma ili kutumia utaalamu wao kuleta matokeo chanya.

Amesema watumishi wahakikishe wanawasikiliza wananchi na wasiwafukuze maofisini badala yake waende Vijijini kuwaeleza fursa ambazo zinatekelezwa na Idara mbalimbali kama Afya na kilimo.

"Shirikianeni na Madiwani kuwafikia wananchi na waelezeeni mafanikio ya Serikali, nendeni kwa wananchi mkawape huduma na kusikiza kero zao".

Waziri Mkuu akaendelea kusema kwamba kumekuwepo na changamoto ya usimamizi  wa vyanzo vya mapato hivyo kusababisha upotevu na hasara kwa Serikali hivyo kuwataka wakuu wa Idara kutekeleza majukumu yao na kila Idara ihakikishe inafanya kazi yake ili kuleta mabadiliko.

Waziri Mkuu amewataka Maafisa Tawala wa Wilaya kuhakikisha kwamba watumishi wanatekeleza majukumu yao na wanakuwa na maadili ndani ya Halmashauri na kuwachukulia hatua wote watakaokwenda kinyume.

Katika hatua nyingine ameeleza kuhusu utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na kulinda miradi ya maji ambayo Serikali imetumia fedha nyingi kuitengeneza.

Waziri Mkuu amezitaka kamati za maji na Mazingira kusimamia vyanzo vya maji na kuzuia uharibifu wa  Mazingira ili kuongeza upatikanaji wa maji kama ilivyokuwa awali.

Aidha amesema awali maji yalikuwa yakitiririka maeneo mengi katika Kata hiyo lakini kwa sababu mifugo imekuwa ikiingizwa katika vyanzo vya maji na kwenye hifadhi za mazingira.

Amesema Misigiri imekuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji kwa muda mrefu  lakini changamoto hiyo itakwisha  kwa kuwa mradi wa maji umekamilika hivyo kila nyumba utapata maji alisisitiza Waziri Mkuu.

Katika mwaka wa fedha wa 2021/22 Serikali imetenga Bilioni 5.1 kwa aji ya miradi ya maji katika Wilaya ya Iramba ikiwa ni pamoja na mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria aliendelea kueleza Waziri Mkuu.

Mwisho


No comments:

Post a Comment