WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, ameyataka mabaraza ya Madiwani nchini, kupitia vikao vyake kuhakikisha yanafanya maamuzi sahihi yenye tija kwa jamii, badala ya maslahi binafsi yanayosababisha mivutano isiyo na tija.
Mheshimiwa Ummy amesema hayo leo Disemba 22, 2021 wakati akikagua ujenzi wa kituo cha afya cha Kata ya Ilunda, wilaya ya Mkalama mkoani Singida, ambacho Madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo wanapinga ujenzi wake wakitaka kijengwe Kata ya Gumanga huku maagizo ya Serikali yakiwa kijengwe Kata ya Ilunda.
Waziri Ummy, amesema kituo hicho ni muhimu kwa Kata ya Ilunda kutokana na eneo hilo kukosa huduma sahihi za afya kwa muda mrefu na kitahudumia Kata Nne zilizopo wilayani humo.“Niwaombe waheshimiwa Madiwani tuache mivutano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo sisi tulichagua kituo cha afya kijengwe katika Kata ya Ilunda kwasababu kitahudumia Kata Nne. Tunaangalia kipi kitaleta tija ya haraka. Tunajua maamuzi yanafanywa na mabaraza ya madiwani lakini tufanye maamuzi yenye tija.” Amesema Mhe. Ummy Mwalimu
Aidha kutokana na mvutano huo uliokuwa ukichelewesha ukamilishwaji wa kituo pamoja na uidhinishaji wa fedha za ujenzi huo kutoka benki, Waziri Ummy akamwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko, kuhakikisha anachukua jukumu hilo, ili mradi uweze kukamilika kwa wakati.
“Nafahamu mpaka leo (22/12/2021) Mwenyekiti amekataa kusaini mikataba ya ujenzi, Mimi nampa mamlaka Katibu Tawala wa Mkoa ya kusaini. Hatuwezi kuchelewesha ujenzi wa kituo hiki wakati fedha imekuja tangu mwezi wa Nane”. Alisisitiza Mhe. Ummy Mwalimu
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge, amemhakikishia Waziri kuwa Ujenzi wa kituo hicho utakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi pamoja na miradi mingine ya maendeleo inayoendelea kujengwa nkoani humo.Hata hivyo amemshukuru na kumpongeza Waziri wa TAMISEMI kwa kuhitimisha ziara yake ya siku TATU ya kukagua Miradi ya maendeleo, Elimu, Afya na Miundombinu sambamba na kikao na Sekretarieti ya Mkoa pamoja na vikao na mabaraza ya Madiwani katika halmashauri za Mkoa.
Nao wananchi wa Kata hiyo akiwemo Hawa Gyimbi, Oscar Daudi na Josephine Maige, wamefurahishwa na uamuzi huo unaoenda kumaliza tatizo la kufuata huduma za afya umbali mrefu jambo ambalo lilikuwa likiwatesa kwa miaka mingi.
Katika hatua nyingine, Waziri Ummy, amewapongeza Watendaji wa Halmashauri hiyo pamoja na Mkoa kwa jitihada walizozifanya kuhakikisha ujenzi huo unaendelea kwa kasi na kuwataka ukamilishwaji kwa wakati ili huduma za afya zianze kutolewa kwa wananchi hao.
Halmashauri
ya Wilaya ya Mkalama yenye jumla ya zahanati 34, vituo vya afya vinne na
hospitali mbili, ilianzishwa mwaka 2013, baada ya kugawanya kutoka wilaya ya
Iramba.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment