Thursday, November 18, 2021

Mganga Mkuu wa Mkoa Singida akutana na viongozi wa Kanisa Katoliki kujadili mkakati wa uhamasishaji kuhusu chanjo ya UVIKO 19

Jumla ya watu waliopata chanjo kwa mkoa wa Singida ni 26,739 kati ya 1,754,37 ambapo wamekwisha maliza dozi ya Janssen sawa na asilimia 1.5

Akiongea wakati akifungua mkutano wa viongozi wa Kanisa katoliki Jimbo la Singida  uliohusu  uhamasishaji wa chanjo ya corona kwa watanzania mganga  mkuu wa mkoa wa Singida Victorina Ludovick, amesema kumekuwepo na jitihada mbalimbali za kuwafikia wananchi wa makundi yote ili kupata chanjo, ambapo  mbinu mbalimbali zimetumika kuifikia jamii.

Aidha amesema uzoefu walioupata katika hatua za awali unaonesha kuwa elimu kwa umma imechangia mafanikio makubwa katika zoezi hili na kwamba bado ipo haja ya kuwashirikisha waumini wengi ili watambue umuhimu wa kupata chanjo.

Hata hivyo Dkt. Ludovick amefafanua kwamba Wizara ya Afya imepitisha mbinu na mikakati mbalimbali kuhamasisha  mkakati harakishi na shirikishi wa kushirikisha taasisi mbalimbali, makundi ya kijamii  na viongozi wa  dini.

“Kupitia mkutano huu nina imani kubwa kwamba mtaendelea kuwa sehemu inayohubiri kuhusu afya bora kwa wananchi wetu ili kuepusha vifo zaidi vinavyotokana na corona” alisema Victorina Ludovick

“Natambua pia kuwa mbinu zingine za kukabiliana na ugonjwa huu zikiwemo kuvaa barakoa, kutumia vitakasa mikono, kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka pamoja kuzingatia afya ya ulaji vyakula vyenye kujenga kinga za mwili mmekuwa mkizihamasisha kila mkutanapo  kwa waumini wenu”. Aliendelea kufafanua Mganga Mkuu

Hata hivyo Mganga Mkuu amebainisha kuwa kwa sasa chanjo mpya imeingia mkoani hapa aina ya Sinopharm ambayo hutolewa dozi mbili (2) ambapo amewataka wananchi wote waliopata dozi moja ya aina hiyo kuhakikisha wanamalizia dozi ya pili kulingana na maelekezo waliyopewa.

Dkt. Ludovick ameendelea kusema kwamba Chanjo hizo zinatolewa kwa mgawo duniani na wananchi wanazipata bure kupitia vituo maalum vya chanjo, ambapo zimeshapelekwa katika vituo vyote vya huduma za afya nchini. Aidha ameeleza kwamba huduma  hii  inapatikana katika maeneo mbalimbali kwa njia ya huduma mkoba (outreach), maeneo hayo ni pamoja na vituo vya usafirishaji, masokoni, vivukoni, mipakani na maeneo mengine mengi yenye mwingiliano mkubwa wa watu kwa wakati mmoja.

Bado idadi ya watu wanaohitaji chanjo ni kubwa kote duniani hivyo ni  muhimu Tanzania nasi kuhakikisha mgawo wetu tunautumia vizuri na kwa kuzingatia muda wa chanjo hizi kutumika. Alieleza Mganga Mkuu.

Akimalizia hotuba yake amesema kwamba  Chanjo hizo ni salama, zimeonesha mafanikio makubwa na ni njia ya haraka ya kupunguza makali ya ugonjwa wa Corona hivyo kutozipatia umuhimu ni sawa na kujiumiza wenyewe na ni jukumu letu kuwafungua macho wengine ambao bado wana wasiwasi ili wachanje na hivyo kujilinda wao wenyewe na kuwalinda wengine wanaowazunguka. Alimazia Dkt. Victorina Ludovick

Kikao hicho kilihudhurwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Singida, Muwakilishi wa baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), mwezeshaji kutoka Chuo Kishiriki cha Sayansi ya Tiba Muhimbili, Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, AMREF Health, Wadau wa sekta ya Afya na Masista.



No comments:

Post a Comment