Monday, September 20, 2021

Dkt. Mahenge Afanya Ziara Kwenye Masoko Kubaini Changamoto Na Kero Za Wamachinga.

 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Binilith Mahenge leo amefanya ziara katika masoko na mitaa ya  manispaa ya Singida ili kubaini hali halisi  ya maeneo hayo na changamoto zinazowakabili  wafanya biashara wadogo  maarufu kama wamachinga.

Ziara hiyo iliyoshirikisha Kamati ya Usalama ya mkoa na viongozi mbalimbali wa manispaa hiyo ililenga kubaini maeneo yenye changamoto kwa wafanya biashara wenye maduka na wanaopanga bidhaa barabarani.

Akiwa katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa amewataka  wakurungezi na wakuu wa wilaya kuhakikisha zoezi la kuwahamisha wafanyabiashara hao linafanyika kwa njia ya majadiliano badala ya kutumia nguvu.

Aidha Dkt. Mahenge amemshauri Mkurungezi wa Manispaa ya Singida mjini ashirikiane na vyombo vingine ikiwemo TARURA  ili walete mapendekezo ya maeneo tarajiwa pamoja na mipango ya namna ya utekelezaji.

Hata hivyo amebainisha kwamba maeneo tarajiwa lazima yaandaliwe vizuri ikiwemo ujenzi wa vyoo, uwepo wa umeme na maji ili maeneo hayo yawavutie wafanyabiashara.

Aidha amesema mchakato wa kubaini maeneo mapya ya kufanyia biashara na mipango ya kufunga baadhi ya Barabara  kwa nyakati tofauti  inafanyika ili kuhakikisha kila mfanya biashara anaendelea na shughuli zake bila kubughuziwa.

“Nashauri wafanyabiashara wa mjini ambao watatakiwa kupisha maeneo waliopo watafutiwe mengine upande wa huko mjini na wafanyabiashara wa mitaani watafutiwe maeneo  karibu na mitaa yao.” alisema Dkt. Mahenge

 Hata hivyo amewataka wataalamu mbalimbali waliofuatana nao kutumia fursa hiyo kufanya mipango miji wakati wa kufungua maeneo mapya kwa ajili ya biashara.

Ametoa wito kwa wakurugenzi na wakuu wa wilaya kushirikiana ili kuhakikisha zoezi la kuwapanga wafanyabiashara hao halichukui muda mrefu iwe wameshapatiwa maeneo mapya ya bishara kwa njia ya majadiliano.

Ziara hiyo ilifanyika katika kata ya Ipembe barabara Nyerere, Lumumba, sokoni na Posta ambapo kata ya majengo   ilifanyika ziara barabara ya usafirishaji, Ukombozi na Kituo cha mabasi cha zamani.

 Wakati kata ya mandewa ilifanyika maeneo ya Ginnery kuelekea hospitali ya manispaa.

Dkt. Binilithi Mahenge akiwa katika ziara kwenye soko la Kariakoo  manispaa ya Singida mjini kuangalia changamoto na kero  za wamachinga

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Bi Dorothy Mwaluko (aliyeshika kitambaa) akitoa ufafanuzi kwenye baadhi ya mambo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa huo.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Bi Sophia Kizigo (kulia ) akijadili jambo na Mkurugenzi mtendajia Halmashauri hiyo  Bi  Asia Juma Messos wakati wa ziara ya Mkuu wa mkoa iliyofanyika katika Kata tatu za manispaa ya Singida mjijni

No comments:

Post a Comment