Uongozi
wa Kampuni ya Mabasi ya Sumry ya Sumbawanga, Rukwa umetoa ubani wa Sh5.5
milioni kwa familia za ndugu na jamaa waliofariki dunia kutokana na ajali ya
moja ya mabasi yake iliyotokea Aprili 28 katika Kijiji cha Utaho, Wilaya ya
Ikungi, Singida.
Katika
ajali hiyo, watu 19 wakiwamo polisi wanne, walifariki papohapo baada ya
kugongwa na basi hilo lililokuwa likitoka Kigoma kwenda Dar es Salaam.
Ajali
hiyo ilitokea baada ya ajali ya kwanza iliyolihusisha lori na mwendesha
baiskeli ambaye alipoteza maisha katika eneo hilo baada ya kugongwa na lori
hilo. Wakazi hao waliogongwa walikuwa wamekusanyika kushuhudia ajali hiyo.
Basi la Sumry lililosababisha ajali kijiji cha Utaho wilaya ya Ikungi na kuuwa watu 19.
Kaimu
Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Hipoliti Daniel Kholani alisema rambirambi hiyo
ilikabidhiwa kwa Serikali ya Kijiji na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone
ambaye naye alichangia Sh100,000.
Kholani
alisema pia Mbunge wa Singida Magharibi, Mohamed Missanga ametoa Sh600,000 na
wakazi wa Tarafa ya Ihanja waishio jijini Dar es Salaam pia wamechanga
Sh600,000.
“Tangu
kutokea kwa ajali hiyo kijiji kimeendelea kupata idadi kubwa ya wageni kutoka
sehemu mbalimbali kuja kutoa pole kwa wafiwa. Tunatarajia kufanya sala maalumu
kwenye eneo la tukio kesho (leo), kuwaombea ndugu zetu.”
Kholani
alisema wakazi wa kijiji hicho, Mussa Mohammed, Suku Abdallah na Ayubu
Ramadhani bado wamelazwa hospitalini wakiendelea kutibiwa majeraha waliyoyapata
kwenye ajali ya basi hilo ambalo bado lipo Kituo cha Polisi Ikungi.
Picha na taarifa kutoka gazeti la Mwananchi.
No comments:
Post a Comment