Mwanafunzi wa darasa la
sita katika shule ya msingi mchanganyiko Ikungi wilaya ya Ikungi, Julius
Charles, akionyesha umahiri wake katika kutumia vidole vya mguu wa kulia
kuandika viruzi herufi kubwa na ndogo.Mwanafunzi huyo ambaye hana mikono,
anafanya vizuri katika masomo yake.
Wanachama wa klabu ya waandishi
wa habari mkoa wa Singida (Singpress) wameadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya
habari duniani kwa kutoa msaada wenye thamani ya zaidi ya shilingi laki nane
kwa wanafunzi wenye ulemavu mbalimbali wakiwemo wenye ulemavu wa ngozi
(albino).
Wanafunzi walionufaika na msaada
huo ambao ni pamoja na sembe kilo 100,sukari kilo 50 na mchele kilo 150 ni wa
shule ya msingi mchanganyiko Ikungi wilaya ya Ikungi mkoani Singida.
Akizungumza kwenye hafla ya
kukabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa Singpress,Seif Takaza amesema katika
kuadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani mwaka huu,klabu ya Singpress
kwa dhati kabisa imeamua kushirikiana na wanafunzi walemavu wa shule ya msingi
mchanganyiko Ikungi.
Mwalimu mkuu wa shule
ya msingi mchanganyiko Ikungi wilaya ya Ikungi, Olivary Kamilly (wa pili kulia)
akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wananchama wa Singida Press Club
(Singpress).Wa tatu kulia ni mwenyekiti wa Singpress, Seif Takaza na wa kwanza
kushoto ni mweka hazina wa Singpress na anayefuatia ni makamu mwenyekiti
Damiano Mkumbo.
Akifafanua,Takaza amesema lengo
na madhumuni ni kuwapatia wanafunzi walemavu zawadi na msaada mbalimbali ya
kibinadamu ili waendelee kuamini kuwa na wao ni sehemu ya Watanzania.Vile vile
kuwapunguzia makali ya maisha.
“Pia tunatarajia wanafunzi na
walimu wa shule hii ya Ikungi,leo wanaweza kutumia fursa ya uwepo wetu kupaza
sauti zao kwa kutoa chanagamoto na kero zinazowakabili,ili sisi tuweze kutekeleza
jukumu letu la kuyaanika hadharani na jamii na serikali kwa ujumla iweze
kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu”amesema Takaza ambaye ni mwandishi wa habari wa
gazeti la Mtanzania kwa mkoa wa Singida.
Akiongezea nguvu hoja yake
hiyo,amesema waandishi wa habari wakiwemo wa Singpress jukumu lao ni
kufichua,kuonya,kuelimisha,kuburudisha na kukemea aina yoyote ya
ukatili,unyanyasaji na unyanyapaa wanaofanyiwa watu wenye ulemavu.
Awali mwalimu wa shule
hiyo,Olivary Kamilly alitaja baadhi ya changamoto wanazozikabili kuhusiana na
wanafunzi walemavu,ni kukosekana kwa mafuta maalum ya ngozi (skin lotion),kupatikana maji kwa uhakika
hapa shuleni na ukosefu wa kompyuta maalum kwa wanafunziwenye ulemavu wa
macho,ili kwenda na mfumo wa mawasiliano uliopo hivi sasa duniani.
Makamu mwalimu mkuu wa
pili kitengo cha walemavu katika shule ya msingi mchanganyiko Ikungi,Donard
Adamu Bilali, akizungumza na wanachama wa Singida Press Club, waliotembelea
shule hiyo na kutoa msaada wa zaidi ya shilingi laki nane, ikiwa ni sehemu ya
maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari.
Aidha,amesema matarajio yao ni kuongeza
ufanisi zaidi katika kuwasaidia wanafunziwenye ulemavu waweze kujitegemea na
kuonyesha vipaji vyao katika kujenga maisha yao.
“Pia tunawapatia mafunzo ya ujasiriamali wanafunzi wenye
ulemavu,ili kupunguza
utegemezi pindi wamalizapo masomo
yao”,amesema mwalimu Kamilly.
Mkuu
huyo wa shule,ametumia fursa hiyo kuipongeza klabu ya waandishi wa habari mkoa
wa Singida,kwa uamuzi wao wa kiungwana kwa kuwasaidia wanafunzi walemavu ambao
wapo kwenye kundi la watu wenye mahitaji maalum.
“Naomba
nitumie fursa hii adimu,kuziomba asasi mbalimbali na watu binafsi kuiga mfano
wa Singpress.Tuondoe dhana potofu kuwa misaada inatolewa na matajiri,makampuni
makubwa au kutoka nje ya nchi,bali tushikamane sisi wenyewe bila kujali uwezo,tusaidie
makundi haya hata kama msaada ni mdogo kiasi gani”amesema.
Kwa
mujibu wa mwalimu Kamiily shule hiyo imeanzishwa mwaka 1944 kwa lengo la kutoa
elimu ya msingi ya kawaida.Mwaka 1980,ilibadilishwa na kuwa shule ya msingi
mchanganyiko ambapo kwa sasa ina wanafunzi 1,200 kati yao walemavu ni 104.
Taarifa/picha na Nathaniel Limu, Singida.
No comments:
Post a Comment